Na Mwandishi Maalumu
Mhe. Salma Kikwete, Mlezi wa MEWATA;
Mhe. Kebwe Steven Kebwe (Mb.), Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii;
Mhe Fatma Mwasa, Mkuu wa Mkoa wa Tabora;
Wakuu wa Wilaya – Tabora, Nzega na Urambo;
Wabunge Wote wa Mkoa wa Tabora Mliopo;
Dkt. Serafina Mkuwa, Mwenyekiti wa MEWATA;
Wawakilishi wa Washirika Wetu wa Maendeleo;
Dkt. Joseph Komwihangiro, Mwakilishi wa Marie Stopes;
Madaktari Wote wa MEWATA na Watumishi wa Sekta ya Afya;
Mwakilishi wa Shirika la Marie Stopes na Wawakilishi wa Mashirika Yasiyo
ya Kiserikali Waliopo;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Shukrani na Pongezi
Niruhusuni nianze kwa kuwashukuru Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashid (aliyewakilishwa hapa leo na Naibu Waziri
Mhe.Dkt. Stephen Kebwe) na Mwenyekiti wa Chama cha Madakatari Wanawake Tanzania
(MEWATA), Dkt. Sarafina Mkuwa kwa kunialika kuja kuzindua huduma za uchunguzi
wa saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti Mkoani Tabora. Nawapongeza nyote kwa maandalizi mazuri kwani
ni ukweli usiopingika kuwa shughuli hii imefana sana. Aidha, nawashukuru wenyeji wetu wa Mkoa wa
Tabora wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Fatma Mwasa, kwa mapokezi mazuri
mliyonipatia mimi, mke wangu na wageni wenzetu. Sikutegemea kupata mapokezi
tofauti na haya hapa Tabora, kwani upendo wenu kwangu na ukarimu wenu tunaujua
na unasifika na wengi.
Madhumuni ya Ziara
Ndugu
Wananchi;
Nimekubali kuja kujumuika nanyi katika uzinduzi huu,
siku ya leo, ili kuongeza sauti yangu na uzito kuhusu shughuli hii muhimu na
adhimu inayofanywa na Madaktari Wanawake hapa nchini. Ni ukweli ulio wazi kuwa MEWATA imesaidia
kuokoa maisha ya akinamama wengi nchini ambao, vinginevyo, wangepoteza uhai kwa
saratani hizi mbili zinazowapata wanawake.
Hatuna budi kuvunja ukimya na kuungana na Madaktari Wanawake kuzungumzia
maradhi haya na kuelimishana ili wananchi, wadau na Serikali kwa umoja wetu au
mmoja mmoja, tuchukue hatua stahiki za kukabiliana na maradhi haya.
Aidha, ni nafasi nzuri ya kutoa pongezi zangu kwa
wanachama wa MEWATA kwa kazi kubwa na nzuri waifanyayo na mafanikio yaliyopatikana. Sijui hali ya maradhi haya ingekuwaje hapa
nchini kama Madaktari Wanawake wasingeamua kufanya kazi hii njema
wanayoifanya. Kwa niaba ya wanawake na
wanaume wote wa Tanzania tafadhali pokeeni pongezi zetu za dhati. Endeleeni kufanya kazi hii njema na Mwenyezi
Mungu atawalipa kwa wema wenu na mioyo yenu ya huruma. Nawaahidi kuendelea kuwaunga mkono kwa hali
na mali na kwa kadri ya uwezo utakavyoniruhusu.
Nimefurahi sana kwamba ndugu zetu wa MEWATA wameweza
kufika hapa Tabora siku ya leo. Mtakumbuka
kuwa nilipokuja kwenye Sherehe za Siku ya Wanawake Duniani tarehe 8 Machi, 2010,
niliahidi kwamba nitawaomba MEWATA waje kufanya uchunguzi wa saratani za mlango
wa kizazi na matiti kwa akinamama.
Hayawi hayawi leo yamekuwa.
Nawashukuru sana viongozi na wanachama wa MEWATA kwa kuja kwenu. Mmenitoa kimasomaso. Wahenga walisema: “Ada ya Mja kunena,
muungwana na vitendo”. Ndugu zangu wa
Tabora ahadi imetimia, kazi kwenu. Jitokezeni
kwa wingi kupima muokoe maisha yenu.
Hali ya Magonjwa ya
Saratani ya Wanawake Nchini
Ndugu Wananchi,
Tanzania inatambulika kuwa ni moja ya nchi zenye
kiwango kikubwa cha maradhi ya saratani ya mlango wa kizazi hapa Afrika ya
Mashariki. Inakadiriwa kuwa takriban wanawake
56 katika kila wanawake 100,000 hupata saratani hii. Inakadiriwa
pia kuwa zaidi ya watu 35,000
wanapata saratani hii kila mwaka na zaidi ya watu 27,000 hupoteza maisha. Mwaka 2010 peke yake, wanawake wapatao 6,000 waligundulika kuwa na saratani ya
mlango wa kizazi na wanawake 4,000
kati yao walifariki dunia.
Wataalamu wanatuambia kuwa, saratani hii huwapata
wanawake wa umri wa miaka 30 na 50.
Aidha, wanawake wanaoishi na virusi vya UKIMWI wako katika hatari zaidi
ya kupata ugonjwa huo kwa asilimia 50. Pamoja na tatizo hili, bado tunayo changamoto
ya saratani ya matiti ambayo ni ya pili kwa kusababisha vifo vya wanawake wengi
nchini. Hivyo basi, hapa nchini wanawake
wako kwenye hatari kubwa ya kufa kwa saratani kuliko wanaume kwa sababu
saratani nyinginezo, hazibagui ukiacha ile ya tezidume inayowapata wanaume
pekee.
Hatua za Tahadhari za Kuzingatiwa
Bahati nzuri, saratani ya mlango wa kizazi na saratani
ya matiti zinaweza kutibika ikiwa zitagunduliwa mapema. Njia pekee ya kuweza kugundua mapema ni
kupima mara kwa mara. Wataalamu
wanashauri kuwa ni vyema wanawake wenye umri wa kati ya miaka 30 na 50
wakachunguza afya zao walau mara moja katika kila miaka mitatu. Na, kwa wanawake wanaoishi na virusi vya
UKIMWI wanashauriwa kuchunguzwa walau mara moja kwa mwaka.
Bahati mbaya sana, uzoefu umeonyesha kuwa wanawake
wengi hufika hospitali wakati ambapo ugonjwa umeshapea na kuenea sehemu
nyingine za mwili. Wanakwenda hospitali wakati
maradhi yamefikia hatua isiyoweza kutibika na hivyo kupoteza maisha. Hivyo basi, kupima na kugundulika mapema kwa
saratani ni hatua muhimu sana ya kuepusha vifo vinavyotokana na maradhi hayo.
Bahati nzuri hivi karibuni kumekuwepo na mwamko na mwitikio mzuri wa kujitokeza
kwa wanawake wengi kupima saratani ya matiti.
Haya ni matunda ya kazi nzuri inayofanywa na MEWATA. Juhudi hizi zinapaswa kuendelezwa. Zinastahili kuungwa mkono.
Hatua Zinazochukuliwa na Serikali
Ndugu Wananchi;
Serikali imechukua
hatua mbalimbali katika kukabiliana na saratani ya mlango wa kizazi. Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii imeanzisha Programu inayoshughulikia masuala ya
Saratani za Uzazi katika Kitengo cha Afya ya Uzazi na Mtoto mwaka 2008. Kupitia
programu hii tuna Mpango Mkakati wa Kukinga na Kudhibiti Saratani ya Mlango wa
Kizazi (2011-2016). Mwongozo wa kutoa
huduma umeandaliwa pamoja na miongozo ya
mafunzo kwa watoa huduma na ujumbe wa kuelimisha jamii kupitia njia mbalimbali.
Kupitia programu hii tumeweza kuanzisha vituo zaidi ya 130 vinavyotoa huduma ya
uchunguzi wa Saratani ya Mlango wa Kizazi katika Mikoa 17 hapa nchini. Ukilinganisha na mwaka 2008 tulipokuwa na
vituo vinne tu vilivyokuwa vinatoa huduma hii ya uchunguzi wa Saratani ya Mlango
wa Kizazi na tiba ya mabadiliko ya awali, haya ni maendeleo makubwa.
Ndugu Wananchi,
Kupitia Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii, Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali
wakiwemo MEWATA, Marie Stopes, WAMA na wengineo kutekeleza mpango wa “Utepe wa
Pinki na Utepe Mwekundu” yaani “Pink
Ribbon Red Ribbon”. Kupitia program
hiyo, kampeni ya uchunguzi wa saratani
ya mlango wa kizazi na matiti ilizinduliwa katika mkoa wa Mwanza mwezi Machi
mwaka huu katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Kupitia
mpango huo, tumekabidhi mashine 16 za kutolea huduma za matibabu ya mabadiliko
ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi
(Cryotherapy machine) kwa mikoa ya Mwanza, Mara, Iringa, Njombe na Mbeya. Mipango
inaendelea kwa mikoa iliyosalia pamoja na Tabora kupatiwa mashine hizo
kuendeleza juhudi za Serikali kupanua upatikanaji wa huduma hizi katika mikoa
yote nchini.
Lengo letu
katika kufanya hivyo ni kutaka kupunguza mzigo mkubwa unaoielemea Hospitali
yetu ya kuu kansa ya Ocean Road. Pia, tunataka
kuwapunguzia wanawake adha na gharama ya kusafiri umbali mrefu hadi Dar es
Salaam kwa ajili ya uchunguzi. Tunatambua
umuhimu wa huduma hizi kuwa karibu zaidi
na walipo watu ili ziwafikie wanawake wote bila kujali hali zao za kipato.
Ndugu Wananchi;
Katika
jitihada za kutokomeza maradhi haya, Serikali, kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo,
imeanza kutoa chanjo ya kuzuia Saratani ya mlango wa Kizazi ya “Human Papilloma
Virus (HPV)”. Chanjo hii hutolewa kwa
watoto wa kike wenye umri wa miaka 9. Chanjo
hii hukinga wasipate maambukizi ya virusi ambavyo husababisha Saratani ya Mlango
wa Kizazi. Wizara ya Afya tayari imezindua mpango huo wa utoaji wa chanjo ya
HPV kwa wasichana tarehe 29 Aprili, 2014 wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Chanjo
Duniani na mama Salma Kikwete. Mpango huo ulizinduliwa kwa Halmashauri tano za Hai,
Siha, Moshi Vijijini, Moshi Mjini na Rombo za Mkoa wa Kilimanjaro, kuashiria
kuanza kwa utekelezaji wa azma ya kutoa chanjo hii nchi nzima ifikapo mwaka
2016.
Shukrani kwa Wadau
Ndugu Wananchi;
Napenda
kutoa pongezi na shukrani za pekee kwa MEWATA kwa kazi nzuri na kubwa ya kukuza
uelewa wa jamii na kuhamasisha uchunguzi wa saratani zinazowapata wanawake. Ni dhahiri kwamba ili jambo hili lifanikiwe
lazima liwe na mshika bango wake. Bahati
nzuri ndugu zetu wa MEWATA wamejitoa kimasomaso na wamefanya kazi ya Serikali kuwa
rahisi. MEWATA imekuwa inafanya kazi kwa
karibu na Serikali pamoja na wadau wengine katika kuhamasisha jamii kuhusu
masuala ya Saratani ya Matiti na ya Mlango wa Kizazi. Kama nilivyokwisha kusema awali, juhudi hizo
zimewafikia wanawake wengi nchini na kuokoa maisha yao.
Aidha,
napenda kuchukua fursa hii kutambua na kutoa shukrani maalum kwa Shirika la Marie
Stopes na wadau wote ambao wanashirikiana na Serikali katika kupambana na
tatizo hili kubwa la Saratani ya Mlango wa Kizazi. Vilevile, tunawashukuru wale wote wanaotoa
huduma ya afya ya uzazi na mtoto nchini. Napenda kwa mara nyingine tena
kuwahakikishia ushirikiano wa Serikali ya CCM ninayoiongoza kwenu. Ni, dhamira yetu kupunguza na ikiwezekana hata kumaliza kabisa vifo vitokanavyo na Saratani ya Mlango
wa Uzazi na Saratani ya Matiti ambazo kwa kweli zinaweza kuzuilika.
Wito kwa Wananchi
Ndugu Wananchi;
Natoa wito
kwa wanawake wa Tabora kujitokeza kwa wingi kufanyiwa uchunguzi wa saratani hizi na wataalamu walioko hapa. Napenda kuwatoa hofu kuwa saratani ya mlango
wa kizazi na saratani ya matiti siyo magonjwa ya aibu au ya mkosi au uchawi au laana
na wala siyo magonjwa yasiyotibika.
Magonjwa haya huweza kumpata mwanamke ye yote, awe ameolewa au
hajaolewa, awe amezaa au hajazaa, awe tajiri au maskini. Madhali ni mwanamke anaweza kupata. Sharti lake la kupona ni kugundulika mapema
na kuanza tiba mapema. Kuchelewa
kugundulika na kuchelewa kuanza matibabu ndiko kunakosababisha vifo kutokana na
maradhi haya. Waswahili wana msemo
usemao, mficha maradhi kifo humuumbua.
Hivyo ndugu zangu kina mama nashauri mfanye uchunguzi mapema, ili kama kuna
tatizo muanze tiba mapema.
Napenda kutumia
fursa hii, kuwaasa akina baba na walezi nao kusaidia katika juhudi za kuzuia na
kutibu magonjwa haya ya saratani ya wanawake.
Mwanamke anayepata magonjwa haya anahitaji matunzo na upendo siyo
masimango na unyanyapaa. Masimango na unyanyapaa huwafanya wanawake waogope
kujitokeza kuchunguza afya zao na kupatiwa tiba kwa kuogopa kubaguliwa au
kuachwa. Magonjwa haya yanatibika. Si
kila mwanamke anayepata saratani hufariki dunia. Kinachotakiwa ni baba na mama kushirikiana
kumpeleka mama kufanyiwa uchunguzi na kupata tiba iwapo atagundulika kuwa na
maradhi. Saratani siyo ugonjwa wa zinaa, hivyo, msiwanyanyapae akina mama bali muwalee
na kuwatunza ili waweze kurejea katika hali zao za kawaida. Akina baba muwe ndiyo nguzo ya mafanikio
katika mapambano dhidi ya saratani.
Na, kwa
wanaume wenzangu, tujenge mazoea ya kupima afya zetu hususan kuhusu saratani ya
tezidume (prostate). Hii ni saratani
inayoua wanaume wengi duniani na hapa nchini.
Lakini nayo kama zilivyo saratani za matiti na mlango wa kizazi
zinatibika kama zitagundulika mapema. Kila
mkienda kupima afya pimeni afya ya tezidume mjue mustakabali wenu.
Ndugu Wananchi;
Sote
tukiungana pamoja tunaweza kutokomeza saratani ya mlango wa kizazi na saratani
ya matiti. Nia ya kutokomeza maradhi
haya tunayo, sababu ya kutokomeza tunayo na uwezo wa kuyatokomeza tunao. Kinachotakiwa ni kuunganisha nguvu zetu
pamoja. Mimi na mke wangu Mama Salma
Kikwete tuko nanyi na tutaendelea kuwa nanyi bega kwa bega katika vita hii sasa
na hata baada ya kuacha Urais mwakani.
Inawezekana, timiza wajibu wako!
Ndugu Wananchi;
Kwa vile
niko Tabora ni vyema nikatumia nafasi hii pia, kuyazungumzia baadhi ya mambo
niliyoyazungumzia au kuahidi kufanya safari zilizopita. Kwa upande wa barabara, napenda kuwahakikishia
kuwa barabara kuu zinazoendelea kujengwa hapa Mkoani Tabora tutazimaliza. Subira yavuta heri. Barabara ya Urambo –Kaliua ujenzi utaanza mwaka huu wa fedha na
Chaya – Nyahua, mchakato wa kutafuta fedha unaendelea ili nayo ujenzi wake
uweze kuanza kabla ya mimi kumaliza kipindi changu cha uongozi. Kuhusu kupata maji ya Ziwa Victoria, kwa Igunga, Nzega, Tabora, Urambo na Sikonge hatua
za awali zimeanza na kinachofuatia ni kutafuta fedha kwa ajili ya mradi huo
mkubwa. Tunakusudia kuiomba Serikali ya
India ambayo ndiyo iliyogharamia matayarisho ya mradi. Tuna matumaini ya kufanikiwa. Sote tuzidi kuomba iwe hivyo.
Kwa upande
wa tatizo la wakulima wa tumbaku kutokulipwa stahili zao na vyama vya ushirika
nimeelezwa na kulielewa. Kuna tuhuma za
wizi na ubadhilifu. Nimemuagiza Inspekta
Jenerali wa Polisi atume watu wake wa upelelezi wa makosa ya Jinai waje wafanye
uchunguzi ili wahusika wakamatwe na kufikishwa Mahakamani na kupewa adhabu
zinazostahili. Ameniahidi kuwa keshokutwa
Jumatatu watu hao watakuja. Wapeni
ushirikiano unaostahili ili tukomeshe uhalifu na dhuluma zinazofanywa na
Maofisa wa Vyama vya Ushirika na taasisi za fedha kwa muda mrefu sasa.
Baada ya
kusema hayo, naomba nitangaze sasa zoezi hili la uchunguzi wa Saratani ya Mlango
wa Kizazi na ya Matiti limefunguliwa rasmi.
Nawashukuruni
sana.
No comments:
Post a Comment