Tuesday, April 22, 2014

JK AOMBOLEZA VIFO VYA AJALI SIMIYU


JK AOMBOLEZA VIFO VYA AJALI SIMIYU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Dkt.  Jakaya  Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,  Paschal Mabiti, kuomboleza vifo vya watu 11 ambao wamepoteza maisha yao katika ajali ya basi iliyotokea mkoani humo  Aprili 21

Katika salamu hizo, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la kusikitisha  kuwa ajali zabarabarani zinaendelea kuchukua maisha ya watu wasiokuwa na hatia.

“Nimepokea kwa huzuni nyingi taarifa ya ajali hiyo ambayo nimejulishwa kuwa imetokea katika Kijiji cha Itwimila katika Wilaya ya Busega katika Mkoa wako wa Simiyu wakati basi lililokuwa linasafiri kutoka Tarime, Mkoa wa Mara kwenda Mwanza kupitia Simiyu lilipoacha njia na kugonga nyumba kabla ya kupinduka.”

Amesema Rais Kikwete: “Nakutumia salamu zangu za rambirambi na najiunga nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa katika nchi yetu. Aidha, kupitia kwako, natuma salamu za dhati ya moyo wangu kwa familia zote ambazo zimepoteza wapendwa wao katika ajali hiyo. Naungana nao katika kuomboleza wapendwa wao. Napenda wajue kuwa msiba wao ni msiba wangu. Pia, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aziweke peponi roho za marehemu.”

Rais Kikwete pia ametoa pole kwa wote ambao wameumia katika ajali hiyo, akiwaombea wapone haraka na kurejea kwenye shughuli zao za kujiletea maendeleo.

No comments:

Post a Comment