Na Mwandishi Maalumu
RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema
kuwa hana wasiwasi na hali ya mjadala mkali uliotawala Bunge Maalum la Katiba
kwa sababu ni muhimu kwa mjadala kuhusu Katiba Mpya ukawa wa kina ili kuweza
kupata Katiba bora kwa Watanzania.
Aidha,
Rais Kikwete amesema kuwa Katiba ya Tanzania haitapatikana kwa mikutano ya
kisiasa nje ya Bunge Maalum la Katiba bali ndani ya Bunge hilo ambako ni
dhahiri kuwa mjadala utatawaliwa na nguvu ya hoja na busara.
Rais
Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ametoa
ufafanuzi huo mchana wa leo, Ijumaa, Juni 20, 2014, wakati alipotoa Mhadhara (Lecture)
kuhusu Usalama wa Taifa (The Security of the Nation) kwenye
Chuo cha Taifa cha Ulinzi – National Defence College – kilichoko
Kunduchi, Dar Es salaam.
Wakati
wa kipindi cha maswali na majibu, ofisa mmoja wa Jeshi la Kenya alimwuuliza
Rais Kikwete kama alikuwa na wasiwasi kuhusu mjadala unaoendelea nchini kuhusu
Katiba Mpya unaweza kuvuruga usalama wa Tanzania.
Rais
Kikwete amemjibu: “Sina wasiwasi hata kidogo kwa sababu hatukutarajia kuwa mjadala wa Bunge
Maalum la Katiba kuhusu jambo hili kubwa ungekuwa rahisi. Yalipojitokeza maoni
ya Tanzania kupata Katiba Mpya, tuliunda Tume na tume hiyo ikatoa ripoti yake
ambayo ndiyo inajadiliwa katika Bunge Maalum. Hatukutarajia kuwa mjadala kuhusu
ripoti ungekuwa rahisi kwa wajumbe kutoa majibu ya ndiyo ama hapana.”
Ameongeza
Rais Kikwete: “Kinachoendelea ni jambo muhimu na la lazima…najua wakati mwingine
majadiliano yalikuwa makali mno lakini hili ni jambo zuri. Aina ya mfumo na
muundo wa Serikali lilizusha mjadala mkali lakini hayo ni matokeo ya hali
halisi ya masuala yanayojadiliwa.”
“Ni
imani yangu kuwa tutafikia mwisho. Mwisho upi, hilo ni suala la Wajumbe wa
Bunge Maalum la Katiba kuamua. Muhimu ni kwamba Katiba Mpya inaweza kupatikana
kutoka Bungeni tu siyo kupitia mikutano ya hadhara nje ya Bunge. Huko hakuna Katiba
huko kuna mikutano ya hadhara na siasa tu. Katiba itapatikana kwa mijadala na
kwa nguvu ya hoja ndani ya Bunge letu.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU
No comments:
Post a Comment