Na Mwandishi
Wetu:
MAMLAKA ya
Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imekabidhi msaada wa madawati 110 yenye
thamani ya shilingi milioni 20 kwa shule za Mkoa wa Lindi katika hafla
iliyofanyika hivi karibuni katika kijiji cha Mahumbika kilichopo Lindi
vijijini.
Msaada huo wa
madawati umekabidhiwa kwa shule hizo hivi karibuni na mwakilishi wa Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Absolom Bohella mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mh.
Ludovick Mwananzila.
Akizungumza mara
baada ya kupokea msaada huo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mh. Ludovick Mwanzila
ameushukuru uongozi wa TPA kwa msaada huo na kuzitaka taasisi nyingine kuiga
mfano wa TPA katika kuchangia elimu ya Mkoa wa Lindi.
“Napenda
niwashukuru Mamlaka ya Bandari kwa msaada huu lakini pia isiwe mwisho na
niziombe taasisi nyingine ambazo tumeziandikia kuziomba madawati kujitokeza na
kutimiza ahadi walizotupa ili wanafunzi wetu wapate mazingira mazuri ya
kusomea,” amefafanua Mwanzila.
Kwa upande wake
Bw. Bohella ambaye pia ni Mkuu wa Bandari ya Mtwara ameushukuru uongozi wa Mkoa
wa Lindi pamoja na ule wa Chuo cha Veta kwa ushirikiano walioutoa wakati wa
ujenzi na usambazaji wa madawati hayo.
“Pia napenda
kuishukuru Ofisi yako pamoja na uongozi wa Chuo cha Veta kwa kutupa ushirikiano
mzuri wakati wa ujenzi wa madawati haya ambayo kwa kweli yametengenezwa kwa
ubora wa hali ya juu jambo linalodhihirisha kuwa Veta wanaweza,” amefafanua
Bohella.
Mbali na kutoa
misaada kwa jamii, Bohella amekumbusha kwamba TPA inatambua na imejizatiti
kutoa huduma zake kwa ufanisi na viwango vya hali ya juu ili kuinua pato la
Mkoa wa Lindi na Taifa kwa ujumla.
Amesema kwamba
TPA kama zilivyo taasisi nyingine za Serikali zilizopo katika mpango wa
‘Matokeo Makubwa Sasa,’ inatekeleza majukumu yake kwa kasi na ufanisi.
No comments:
Post a Comment