Mheshimiwa
Dkt. Kebwe Stephen Kebwe(Mb) – Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii;
Mheshimiwa
Stanslaus Magesa Mulongo - Mkuu wa mkoa wa Arusha;
Ndugu Paul Magesa - Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania;
Ndugu Clavery Mpandana – Muuguzi Mkuu wa Serikali;
Daktari
Khadija Malima, Mwenyekiti wa Baraza la Wauuguzi Tanaznia na Chama cha Wauguzi Tanzania;
Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nakushukuru sana
Ndugu Rais na viongozi wenzako wa Chama cha Wauguzi na Wakunga (TANNA) kwa
heshima kubwa mliyonipa ya kuja kujumuika nanyi katika maadhimisho ya mwaka huu
ya Siku ya Wauguzi Duniani. Nakupongeza
pia Mheshimiwa Magesa Mulongo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha na wananchi wote wa
Arusha kwa kutupokea vizuri na kwa
kukubali kuwa wenyeji wa sherehe hii na kushiriki kwa ukamilifu katika
kufanikisha maandalizi yake.
Nawapongeza nyote kwa maandalizi mazuri ya maadhimisho haya. Hakika yamefana sana. Nimefurahishwa na maonesho kuhusu baadhi ya shughuli zinazofanywa na wauguzi katika kuwahudumia Watanzania. Maonesho ya aina hii husaidia sana kukuza uelewa wa wananchi kuhusu majukumu yenu, wajibu wenu na mchango wenu katika kuimarisha afya za Watanzania. Pamoja na kutembelea mabanda ya maonyesho, nimeshuhudia maandamano yenu na kusoma ujumbe kwenye mabango ya washiriki. Pia nimesikiliza Risala yenu iliyosomwa kwa ufasaha na utulivu mkubwa na Rais wa Chama cha Wauguzi Ndugu Paul Magesa. Kwa ujumla, maadhimisho haya yanadhihirisha kuwa wauguzi ni kiungo muhimu sana katika utoaji na maendeleo ya huduma ya afya nchini na ni nguvu thabiti ya mabadiliko.
Kauli Mbiu
Ndugu
Rais wa Chama cha Wauguzi;
Ndugu
Wauguzi na ndugu wananchi;
Nilipopata mwaliko kutoka kwenu
sikusita kukubali kuja kujumuika nanyi siku ya leo kwa sababu kuu mbili. Kwanza, kwamba wauguzi ni kada muhimu sana
katika utoaji na maendeleo ya huduma ya afya nchini. Bila ya kuwepo wauguzi huduma ya afya itayumba.
Natambua kuwa Wauguzi ni zaidi ya asilimia 60 ya watumishi wote wa sekta
ya afya na hutekeleza asilimia 80 ya
shughuli zote za afya. Aidha, Muuguzi ndiye mwenye kuandaa mazingira mazuri kwa
daktari kutekeleza majukumu yake. Daktari anapomaliza kumuona mgonjwa, na kutoa
maelekezo yake, Muuguzi husimamia utekelezaji wa maelekezo hayo pamoja na tiba
yenyewe. Muuguzi ndiye anayefanya kazi
ya kuuguza mgonjwa. Sote ni mashahidi kuwa wagonjwa wanatumia wakati mwingi
zaidi mikononi mwa wauguzi kuliko muda wanaoutumia mikononi mwa wahudumu
wengine wa afya.
Ndugu Rais wa Chama cha Wauguzi;
Ndugu Wauguzi;
Sababu
ya pili ni kwamba nimevutiwa na kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo;
“Wauguzi ni Nguvu ya Mabadiliko na
Rasilimali Muhimu ya Afya”. Ni kauli mbiu sahihi na mwafaka kabisa. Ni ukweli ulio wazi kuwa wauguzi wanayo
nafasi maalum katika maendeleo ya huduma ya afya na sekta yenyewe kwa
jumla. Ni chachu muhimu ya mabadiliko
katika sekta ya afya, na ndiyo rasilimali ya kuwezesha mabadiliko hayo kutokea
na kufanikiwa.
Huwezi
kuzungumzia mabadiliko katika sekta hii bila kutambua mchango wa Wauguzi na
kuwahusisha. Ujenzi wa miundombinu ya vituo vya kutoa huduma ya afya, ununuzi
na usambazaji wa madawa, ununuzi wa vitendea kazi vya kisasa katika hospitali
zetu vitakuwa na maana tu pale ambapo wauguzi wapo na wanatimiza wajibu wao ipasavyo.
Tunaweza kusema kwa uhakika kabisa kuwa hakuna mbadala wa wauguzi.
Ndugu
Wananchi;
Uangalizi
unaotolewa na wauguzi, upendo na huruma yao husaidia sana kurejesha matumaini
ya wagonjwa na watu wengine wanaojishughulisha na maendeleo ya huduma ya afya.
Huongeza ari ya mapambano dhidi ya maradhi na kuleta matumaini kwamba ushindi
utapatikana. Ninyi ndiyo kioo cha huduma ya afya. Ndiyo watu wa kwanza
mnaokutana na wagonjwa wanapofika hospitali, na ni watu wa mwisho kuwaona
wanapotoka baada ya matibabu.
Mheshimiwa Naibu Waziri;
Rais wa Chama cha Wauguzi;
Ndugu Wauguzi na ndugu Wananchi;
Kuboresha
huduma ya afya ni moja ya vipaumbele vya juu vya Serikali ninayoiongoza na
ndiyo maagizo ya Ilani ya Uchanguzi ya Chama Tawala – CCM. Kwa sababu hiyo
tulipoingia madarakani mwaka 2005 tulitoa umuhimu wa pekee kwa zoezi la kupitia
upya Sera ya Afya ya mwaka 1997 kwa lengo la kuihuisha. Matokeo yake ni
kupatikana kwa Sera Mpya ya Afya ya mwaka 2007 na Mpango wa Maendeleo ya Afya
ya Msingi wa mwaka 2007 uliotengenezwa maalum kuongoza utekelezaji wa Sera hiyo.
Kama
mjuavyo huu ni mpango wa miaka kumi mpaka mwaka 2017 unaolenga kuleta mageuzi
na maendeleo makubwa katika sekta ya afya. Kwa muhtasari tumepanga kufanya mambo makuu
mawili. Kwanza, kusogeza huduma ya afya karibu na wanapoishi wananchi kwa
kujenga na kuimarisha vituo vya kutolea huduma za afya. Pili, kuimarisha ubora
wa huduma ya afya inayotolewa kwa wananchi kwa kuvipatia vituo hivyo vifaa vya
uchunguzi na tiba vilivyo bora pamoja na dawa za kutosha. Pia kuvipatia rasilimali
watu, kwa maana ya Madaktari, Waganga, Wauguzi, Wakunga na Wataalamu wengine wa
afya.
Ndugu Wauguzi na Ndugu Wanannchi;
Leo
miaka karibu saba baadae ninyi ndiyo mashahidi wa mafanikio tuliyoyapata katika
utekelezaji wa Mpango huu. Tumefanikiwa kwa kiasi cha kutia moyo ingawaje bado
tunayo kazi kubwa mbele yetu. Kwanza kabisa tumeongeza sana bajeti ya afya kutoka
shilingi bilioni 271 mwaka 2005/2006
hadi shilingi trilioni 1.4 mwaka 2013/2014. Imekuwa bajeti ya tatu kwa ukubwa baada ya
elimu na miundombinu kutoka ya sita. Kwa
sababu ya ongezeko hilo tumeshuhudia mambo mengi mazuri yakifanyika katika kuboresha
huduma ya afya nchini. Kwa mfano, zahanati
ziko 5,960 ukilinganisha na 4,930 zilizokuwepo mwaka 2007. Vituo vya afya viko 716 ukilinganisha na 565
na hospitali ziko 249 ukilinganisha
na 230 wakati ule.
Kazi
kubwa imefanyika kuimarisha hospitali za Wilaya, Mikoa, Kanda na Hospitali ya
Taifa Muhimbili. Kazi bado inaendelea na tunaweza kusema ndiyo
kwanza imechanganya. Miundombinu imeongezwa na majengo mengine yanaendelea
kujengwa. Huduma zinaendelea kuboreshwa na nyingine ambazo hazikuwepo zimeanzishwa.
Hali kadhalika vifaa tiba na uchunguzi vya kisasa vimeendelea kuwekwa na uwezo
wa hospitali kuchunguza na kutibu maradhi umekuwa mkubwa.
Tumeendelea
kupanua fursa za mafunzo na ajira kwa Madaktari, Wauguzi na Wataalamu wengine
wa afya. Kwa upande wa mafunzo kwa mfano
Madaktari waliojiunga na mafunzo wameongezeka kutoka 520 mwaka 2005 hadi 1,057
hivi sasa. Kwa Wauguzi na Wakunga wameongezeka
kutoka 1,586 mwaka 2005 hadi 3,569 hivi sasa, kwa jumla kila kada
imeongezeka. Ujenzi wa Kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi
Shirikishi cha Muhimbili pale Mloganzila itaongeza sana uwezo wetu wa kufundisha
Madaktari na Wauguzi kutoka Chuo hicho kutoka 3,000 mpaka 15,000. Ukiongeza na wanafunzi 5,000 wa Chuo cha Tiba katika Chuo Kikuu cha Dodoma tatizo la
rasilimali watu nchini litapatiwa ufumbuzi miaka michache ijayo. Tayari ujenzi
wa Hospitali ya Kufundishia ya vitanda 600
umeanza pale Mloganzila. Hospitali
hiyo nayo itaimarisha ubora wa huduma ya uchunguzi na tiba ya maradhi kwa namna
yake hapa nchini. Hali kadhalika ujenzi wa Hospitali ya Kufundishia pale UDOM
unatarajiwa kukamilika mwaka huu.
Hivyo
hivyo, kwa upande wa ajira nako kumekuwa na
ongezeko. Idadi ya Madaktari waliosajiliwa imeongezeka kutoka 1,339 mwaka 2006 hadi 3,133 na Wauguzi kutoka 20,115 mwaka 2007 hadi 34,740 hivi sasa. Aidha, katika kipindi
cha miaka 3 iliyopita, tumeajiri wauguzi 8,659
na tunatarajia kuajiri wengine 1,152
kabla ya Julai, 2014. Tutaendelea kufanya hivyo mwaka ujao wa fedha na miaka
inayofuatia. Hii itasaidia kupunguza mzigo wa kazi mlio nao sasa hivi ambao
mmeutaja kwenye risala yenu.
Ndugu Rais wa Chama cha Wauguzi;
Ndugu Wauguzi;
Kwa
upande wa maslahi nako, tumejitahidi kuboresha, najua bado tunayo kazi kubwa ya
kufanya mbele yetu. Bado mishahara ni midogo
lakini hatujafika mwisho, tunaendelea kuboresha. Tumekuwa tunaongeza kila mwaka na tutaendelea
kufanya hivyo mwaka huu na miaka ijayo.
Risala ya Wauguzi
Ndugu Wauguzi,
Nimesikiliza
kwa makini risala yenu iliyowasilishwa vizuri na Ndugu Paul Magesa, Rais wa
Chama cha Wauguzi na Wakunga. Namna ambavyo ameiwasilisha, lugha aliyotumia kuiwasilisha
na jinsi mlivyoishangilia inathibitisha kuwa risala hii ni shirikishi, na
yaliyosemwa ni mambo muhimu kwa wauguzi kwa ujumla wenu. Ni risala iliyosheheni
ukweli kuhusu mafanikio tuliyoyapata na mambo yanayowatatiza mnayotaka yapatiwe
ufumbuzi. Kuna ushauri mzuri uliotolewa kuhusu nini kifanyike kuboresha
mazingira ya kazi ya Wauguzi na huduma ya afya nchini. Lazima nikiri kuwa nimeguswa
sana na ahadi yenu ya kuendelea kufanya kazi kwa mujibu wa viapo vyenu, licha
ya changamoto zilizopo.
Napenda
kuwahakikishia kuwa Serikali inaelewa mchango wenu muhimu na inauthamini sana
hivyo basi, sisi tutakuwa watu wa mwisho kupuuza mambo ya wauguzi. Kama kuna jambo halijafanyika haitokani na
kupuuza au ukosefu wa dhamira ya kuyashughulikia bali kuna sababu fulani fulani
za msingi zinazotukwaza katika utekelezaji wake.
Nimefurahishwa
sana na dhamira yenu njema ya kutaka kuona mabadiliko yanafanyika katika sekta
ya afya na ninyi kuwa sehemu kamili ya mabadiliko hayo. Ndiyo maana sehemu
kubwa ya risala yenu ina mapendekezo ya mambo ya kubadilisha ili kuboresha
utoaji wa huduma ya afya. Nawaunga mkono kwa
msimamo wenu huo. Nimefarijika sana kusikia kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii na Wizara nyingine za Serikali kuwa mambo mengine yametekelezwa na yapo
ambayo tunaendelea kuyatekeleza. Hata hivyo, bado yapo mambo ambayo tunayavutia
pumzi kwa maana ya kujenga uwezo wa kuyatekeleza.
Ndugu
Wauguzi;
Hii ni mara ya tatu napata nafasi ya
kukutana na kuzungumza na viongozi wa Wauguzi.
Mara ya kwanza ilikuwa Mnazi Mmoja mwaka jana, mara ya pili Ikulu tarehe
29 Aprili, 2014 na leo ndiyo mara ya tatu hapa Arusha. Jambo mojawapo muhimu nililojifunza
ni kuwa mambo mengi yanayowatatiza wauguzi, ambayo pia yameainishwa katika
risala yenu leo, yanaweza kumalizwa kwa kuboresha mawasiliano na mahusiano kati
yenu na Wizara zinazohusika na kati yenu (wauguzi) na kada nyingine katika
sekta ya afya. Naamini kama hayo yakifanyika mambo mengi yatapatiwa ufumbuzi na
kwamba yatabaki machache yanayohitaji msaada wa ngazi za juu. Hii itasaidia
kuondoa kutiliana mashaka, kutokuaminiana na hisia za kupuuzwa kwa wauguzi. Nimeona nitumie fursa ya maadhimisho haya ya
leo kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya masuala tuliyozungumza siku zilizopita na yaliyoibuliwa
hapa leo kwenye mabango na risala.
Madai ya Wauguzi
Ndugu
Rais wa Chama cha Wauguzi;
Ndugu
Wauguzi,
Katika
risala yenu mmezungumzia mambo yahusuyo muundo wa utumishi, mafunzo, posho,
huduma ya makazi na mambo mengineyo muhimu.
Mambo yote haya ni ya msingi na napenda kuwahakikishia kuwa tutayachukulia
kwa uzito unaostahili na tutayafanyia kazi ipasavyo ili tuwatengenezee
mazingira mazuri ya kufanya kazi zenu.
Muundo wa Utumishi wa
Uuguzi
Ndugu
Rais wa Chama cha Wauguzi;
NduguWauguzi;
Kwanza
kabisa nawapongeza kwa kukamilisha mapendekezo ya Muundo wa Utumishi. Nitawasaidia
kufuatilia kwa mamlaka husika ili uamuzi ufanyike mapema iwezekanavyo.
Kukamilika kwa zoezi hilo kutatoa ufumbuzi kwa mambo mengi yanayowatatiza hivi
sasa. Itayaweka sawa masuala ya upandishaji wa vyeo. Itawezesha kutambuliwa ipasayo kwa wauguzi
wanaomaliza shahada za uzamili na uzamivu.
Kwa kweli nashangaa kwa nini watu waliojiendeleza kiasi hicho wapate
taabu ya kutambuliwa inavyostahili katika utumishi wa uuguzi.
Hivyo
hivyo nashangaa tena napata taabu kuamini kuwa mtumishi akienda masomoni
kuongeza ujuzi anasimama kupanda cheo au hata kushushwa cheo. Haya ni ya kustaajabisha mambo ambayo
hayastahili kufanyika. Naomba Wizara na
mamlaka husika zihakikishe kuwa uonevu huu hauendelei kufanyika. Iweje
leo kujiendeleza iwe ni balaa kwa mfanyakazi na mwajiri badala ya kuwa jambo
jema kwa wote.
Ndugu
Wauguzi;
Nadhani
suala la uanzishwaji wa Kurugenzi ya Uuguzi ndani ya Wizara ya Afya limefikia
hatua nzuri. Nimeambiwa kuwa Wizara
iliridhia maombi yenu na kuyawasilisha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma. Wataalamu wa Mifumo katika Idara Kuu ya Utumishi walichoshauri ni kuwa
Sehemu ya Uuguzi sasa ipandishwe hadhi na kuwa Kitengo cha Uuguzi
kitakachoongozwa na Mkurugenzi. Nimeambiwa pia kwamba Wizara ya Afya imekubali
na tayari imefanya marekebisho na kuwasilisha upya pendekezo hilo. Nimesikia kuwa jambo hili litakamilishwa muda
si mrefu na huenda muundo huo ukaanza tarehe 1 Julai, 2014 hivyo kuhitimisha
maombi yenu. Niruhusuni niwapongeze kwa hatua iliyofikiwa mpaka sasa.
Maslahi ya Watumishi
Ndugu
Rais wa Chama cha Wauguzi;
Ndugu
Wauguzi;
Kuboresha
maslahi ya Watumishi wa Umma, hususan mishahara na posho mbalimbali ni mambo ambayo Serikali imeyapa kipaumbele.
Tumekuwa yunafanya hivyo kila mwaka na tutaendelea kufanya hivyo. Maombi yenu tumeyapokea na tutayafanyia kazi.
Napenda kusema hata katika Bajeti ya
mwaka ujao wa fedha hatua kiasi fulani zitachukuliwa.
Nimesikia
kilio chenu kuhusu posho zilizoamuliwa kutokutekelezwa na ile ya sare za kazi ambayo
imeahidiwa na kuongezwa kutoka shilingi
150,000 na kuwa Shilingi 300,000 kutokamilishwa
mpaka sasa. Nitatoa maagizo kwa mamlaka husika katika Serikali kufuatilia na
kuwabana, watakaokaidi. Hivyo hivyo, kwa posho ya kufanya kazi usiku, kama
ilishaamuliwa ilipwe, mamlaka husika zitatakiwa kutekeleza bila ajizi.
Nyumba za Wauguzi
Serikali
inatambua umuhimu wa wauguzi kuwa na makazi karibu na maeneo yao ya kazi. Kwa
kutambua umuhimu huo Serikali imekuwa inatenga fedha za kujenga nyumba za
madaktari na wauguzi kila mwaka. Hata
hivyo kasi ya ujenzi ni ndogo ukilinganisha na ukubwa wa mahitaji kwa sababu ya
ufinyu wa bajeti. Tutatafuta njia
nyingine za kuharakisha ujenzi wa nyumba hizo. Mipango hiyo ikikamilika mtaona matokeo
yake. Kwa sasa tutaendelea na kazi ya
ujenzi wa nyumba katika mikoa ya Mtwara,
Rukwa, Tabora na Mara.
Nimelipokea
pendekezo lenu la kutaka msaidiwe kupata viwanja vya kujenga nyumba. Nitaagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi wawasaidie. Miaka miwili iliiyopita niliagiza utengenezwe
mpango maalum wa mikopo ya nyumba kwa watumishi wa umma. Matayarisho yanaendelea, ukikamilika
utasaidia wafanyakazi wa umma wakiwemo Wauguzi kujipatia nyumba za kuishi.
Udhamini wa Mafunzo
Ndugu Rais wa Wauguzi;
Ndugu Wauguzi,
Nimesikia
rai yenu ya kutaka Serikali itoe udhamini kwa wanafunzi wanaosomea shahada ya
kwanza ya uuguzi kama tunavyofanya kwa
wale wanaosomea udaktari. Nakubali maombi yenu, nitaagiza mamlaka husika
walifanyie kazi. Kama hivi sasa wanafunzi
hao siyo wengi tunaweza kuanza hata bajeti ijayo lakini kama ni wengi itabidi
tuanze mwaka wa fedha wa 2015/16 lazima tujipange vizuri kwani inahusu pesa.
Naamini
uamuzi huu utahamasisha wauguzi kujitokeza kwa wingi kujiendeleza kitaaluma. Wauguzi
wasiishie kwenye Cheti na Diploma bali waende zaidi ya hapo. Napenda kuwahakikishia
pia kwamba pamoja na uamuzi huu, Serikali bado itaendelea kudhamini wauguzi
wanaosomea shahada ya uzamili na uzamivu kama tufanyavyo sasa. Nimesikia utayari wenu wa kupewa nafasi za
uongozi katika Wizara ya Afya na kwingineko kama tulivyofanya kwa Mkuu wa Mkoa
wa Tanga.
Wito kwa Wauguzi
Ndugu
Rais wa Chama cha Wauguzi;
Ndugu
Wauguzi,
Tunapoadhimisha
siku ya wauguzi, tunakumbuka pia siku ya kuzaliwa kwa Bi. Frorence
Nightlingale, mwanzilishi wa taaluma na fani hii adhimu ya uuguzi. Mama
Nightlingale aliyeishi kati ya mwaka 1820 hadi 1910 ndiye aliyeanzisha shule ya
kwanza ya wauguzi huko London katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas. Alianzisha
huduma hii baada ya uzoefu wake katika kuwashughulikia majeruhi wa kivita, na
wanajeshi wagonjwa wakati wa vita.
Sifa
yake kubwa ilikuwa ni wito na moyo wa kujitolea na huruma vitu ambavyo aliamini
ndio misingi ya kuwa muuguzi. Alipata kunukuliwa akisema, “Kama muuguzi atakacha kutoa
huduma kwa sababu yoyote ile au kusema haimuhusu, basi uuguzi kwake sio wito”. Kutokana na maisha yake ya kuwaangazia nuru
wagonjwa na kuwatembelea usiku akiwa na taa ya kandili kuwafariji na
kuwahudumia, alipewa jina la “Mwanamke Mwenye
Kutembea na Nuru”.
Ndugu
Wauguzi;
Ninyi
ni watu wenye dhamana kubwa juu ya maisha ya watu na mnategemewa sana. Nawapongeza
kwa kazi kubwa na nzuri muifanyayo. Kwa sababu yenu mmeokoa maisha ya watu
wengi na kuwapunguzia maumivu wagonjwa. Wakati mwingine moyo wenu kuonyesha
kujali, upendo na huruma hutoa matumaini kwa mgonjwa na kumrejeshea siha yake.
Hivyo, nawaomba muendelee kuwa na kauli nzuri na nyuso zenye tabasamu na nyoyo za
huruma na upendo kwa wagonjwa. Tabia
hiyo ni tiba ya aina yake.
Nimeona
niikumbushe hadithi ya muasisi Mama Florence Nightngale ili kuwaomba wakati
wote iwaongoze na muendelee kukumbushana kuizingatia. Minong’ono kuwa mienendo
ya baadhi yenu inalalamikiwa na wagonjwa kuwa hailingani na mafundisho ya muasisi
wa kazi hii adhimu inanisumbua sana. Kama nilivyosema awali, ninyi ndiyo watu wa
kwanza mnaokutana na mgonjwa akifika hospitali na ni watu wa mwisho anapotoka
hospitali baada ya matibabu. Ikiwa mtakuwa na nyuso za ukatili na ulimi mkali
au wa kebehi, mtakuwa mnawakwaza wagonjwa na hata kuongeza ukali wa maumivu
yao. Wengine wanaweza kukata tamaa na hata kupoteza uhai. Msifanye watu wajutie kufika zahanati au
hospitali. Narudia kuwasihi mzingatie kiapo chenu na maudhui ya kauli mbiu yenu
ya kutaka mabadiliko. Kwa maana nyingine naomba mtambue kuwa kauli mbiu yenu ya
mabadiliko inawahusu na nyie pia kama inavyotuhusu sote. Lazima mabadiliko yaanze na ninyi wenyewe.
Homa ya Dengue
Ndugu
Wananchi;
Kabla
ya kumaliza hotuba yangu naomba nizungumzie ugonjwa mpya wa Homa ya Dengue
uliojitokeza katika jiji la Dar es Salaam hivi karibuni. Huu si ugonjwa asili
kwetu. Ni ugonjwa wa huko Asia na Bara la Amerika lakini ndiyo umeshafika. Kwa mara ya kwanza ugonjwa huu ulijitokeza
Jijini Dar es Salaam mwaka 2010 na kuathiri watu 40 ambao walipatiwa matibabu
na kupona. Ugonjwa huu ulitoweka lakini ukaibuka tena Mei na Juni, 2013
ulipojitokeza tena na kuwakumba watu 172.
Mwaka huu ugonjwa huo umerudia tena kwa kasi kubwa zaidi. Kati ya Januari na Aprili 6, mwaka huu wagonjwa
399 wamethibitika kuugua katika Jiji
la Dar es Salaam. Kati ya wagonjwa hao 322
walitoka Wilaya ya Kinondoni, 61
Wilaya ya Ilala na 16 Wilaya ya Temeke. Kwa bahati mbaya wawili kati
yao walipoteza maisha.
Ndugu
wananchi;
Wataalamu
wa afya wanasema kuna aina tatu za ugonjwa wa dengue. Aina ya kwanza ni Homa ya
Dengue, aina ya pili ni Dengue ya Damu na aina ya tatu ni Dengue ya Kupoteza
Fahamu. Hapa kwetu Homa ya Dengue ndiyo
ugonjwa uliothibitika kuathiri wagonjwa
wote. Homa hii ina dalili kubwa tatu: homa kali ya ghafla, kuumwa kichwa, na
maumivu ya viungo au uchovu. Kwa vile dalili za ugonjwa huu zinafanana sana na
dalili za ugonjwa wa malaria, ipo hatari kwa watu waliozoea kutumia dawa bila
kupima kumeza dawa za malaria wakati wanaugua Homa ya Dengue. Wakifanya hivyo
watahatarisha maisha yao. Natoa wito kwa mtu yeyote anayejisikia dalili hizi
aende hospitali akapimwe; asinywe dawa
bila kupima kama baadhi yetu tulivyozoea. Ni hatari kwa maisha yetu.
Ndugu
Wananchi;
Ugonjwa huu unaambukizwa na mbu aina
ya Aedes akishamuuma binadamu. Tena
huuma mchana. Hatua za kupambana na mbu huyu ni sawa na zile zinazochulikuwa
kupambana na mbu wa Anopheles
anayeambukiza malaria. Watu waendelee
kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa, kupaka dawa za kuzuia kuumwa na mbu na
kuharibu maeneo ya mazalia ya mbu.
Nimetoa maelekezo kwa Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii kuhakikisha kuwa Bohari Kuu ya Madawa ya Serikali (MSD) wanaleta
kits za kupimia maradhi haya (Dengue Rapid Test Kits) za kutosha na
kuzisambaza kwenye hospitali na vituo vya afya. Nimeambiwa hivi sasa vipimo
hivi havipo vya kutosha. Hii ni dharura ya kitaifa ambayo lazima ipewe uzito na
uharaka unaostahili na Wizara ya Afya na Hazina.
Hitimisho
Ndugu
Rais wa Chama cha Wauguzi;
Ndugu
Wauguzi;
Niruhusuni
nimalize hotuba yangu kwa kurudia kuwashukuru kwa kunialika na kwa risala yenu
nzuri. Nimejifunza mengi na kama nilivyosema, nakwenda kuifanyia kazi risala
yenu na yote niliyosikia na kuona yanayohitaji kuchukuliwa hatua. Yale masuala
ya kimuundo na mengineyo nitakwenda kuyakwamua huko yalikokwama, ili
utekelezaji uanze. Yale yahusuyo posho, kama nilivyoeleza, baadhi yake yatashughulikiwa
katika bajeti ijayo na mengine tutaendelea kuyashughulikia kadri uwezo
utakavyoruhusu.
Ninachoweza
kusema kwa uhakika kabisa ni kuwa tunawapenda, tunatambua umuhimu wenu na
tunawathamini sana. Katu hakuna upungufu wa dhamira bali tunakwazwa na uwezo
mdogo wa mapato ya Serikali kuweza kutosheleza
mahitaji yote ya kuboresha huduma ya afya na maslahi kwa watumishi wa afya nchini. Narudia kusisitiza kuwa kamwe sio kutokana na
kukosekana kwa utayari wa kutatua changamoto zinazowakabili wauguzi au
watumishi wengine wa umma.
Upo
ushahidi wa wazi wa juhudi za Serikali ninayoiongoza ya kufanya mambo mengi
makubwa na madogo ya kuboresha mazingira ya kazi kwa kila kada na sekta kadiri
uwezo unavyoruhusu. Mtakubaliana nami kuwa hali ya kada ya wauguzi ilivyo leo,
si sawa na ilivyokuwa miaka 10 iliyopita. Tumepiga hatua kiasi chake lakini
bado tuna safari ndefu na tutaendelea kufanya zaidi. Ni dhahiri kwamba tumesogea kutoka pale
tulipokuwa, ingawa hatujafika tunapodhamiria kwenda. Kwa vile msimamo na
muelekeo wetu ni sahihi, naamini baada ya muda si mrefu tutafika. Penye nia
pana njia. Inawezekana Timiza Wajibu wako.
Mungu Ibariki Afrika,
Mungu Ibariki Tanzania.
No comments:
Post a Comment