Kaimu
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania;
Bibi
Northburga Maskini;
Waziri
wa Kazi na Ajira, Mheshimiwa Gaudensia Mugosi Kabaka(MB);
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu, Divisheni ya Kazi,
Mh. Regina Rweyemamu;
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Sadiki
Meck
Sadiki;
Waheshimiwa
Mawaziri na Wabunge;
Mkurugenzi wa Shirika la Kazi
Dunia (ILO), Kanda ya
Afrika Mashariki, Ndugu
Alexio Msindo;
Viongozi mbalimbali wa Serikali mliopo hapa;
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi,
Ndugu Nicholaus Mgaya;
Ndugu Almas Maige, Mwenyekiti
wa ATE;
Mkurugenzi Mtendaji, Chama
cha Waajiri Tanzania (ATE),
Dr. Aggrey Mlimuka;
Mheshimiwa Abdulrahman
Kinana, Katibu Mkuu wa CCM na Viongozi wa Vyama vya Siasa Mliopo;
Waheshimiwa Mabalozi;
Msajili wa Vyama vya
Wafanyakazi na Waajiri, Ndugu Doroth Uiso;
Wenyeviti na Makatibu wa
Vyama vya Wafanyakazi;
Viongozi wa Vyama vya Siasa;
Ndugu Wafanyakazi wenzangu;
Mabibi na Mabwana;
Shukrani
Awali ya
yote naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa
kutujalia uhai na kutuwezesha kukutana leo katika sherehe za mwaka huu za
kuadhimisha siku ya wafanyakazi duniani.
Aidha, natoa shukrani nyingi kwa Kaimu Rais wa TUCTA Mama Northburga
Maskini na viongozi wenzako kwa heshima kubwa mliyonipa ya kuja kuungana na wafanyakazi
wa Tanzania katika kuadhimisha siku hii adhimu.
Napenda kutumia fursa hii kupitia kwako Kaimu Rais wa
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania, kutoa salamu nyingi za pongezi na
mkono wa heri kwa wanachama na Viongozi
wa Vyama Vyote vya Wafanyakazi katika
kuadhimisha siku hii kubwa na adhimu. Nawapongeza sana Chama cha Wafanyakazi wa
Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti (RAAWU) kwa
kuratibu vizuri maadhimisho ya mwaka huu. Nimefurahi kusikia kuwa maadhimisho
ya mwaka huu yamehusisha wiki ya wafanyakazi ambako kumekuwa na maonyesho ya
waajiri na wafanyakazi. Huu ni utaratibu mzuri ambao licha ya kuongeza hamasa kwa
maadhimisho haya lakini pia umetoa fursa kwa wananchi wengi kujionea wenyewe
mambo muhimu mnayoyafanya wafanyakazi.
Nitakuwa mwizi
wa fadhila nisipowapongeza na kuwashukuru wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa
na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Saidi Meck Sadiki kwa kukubali kuwa wenyeji wa
sherehe hii. Si kazi rahisi hata kidogo,
hivyo wanastahili pongezi zetu kwa kufanikisha vyema shughuli hii. Tumeona
jinsi uwanja ulivyofurika na maandamano yalivyofana. Usione vinaelea vimeundwa. Tafadhali pokeeni pongezi zetu sote.
Pongezi kwa Wafanyakazi Bora
Wafanyakazi Wenzangu,
Kwa mara
nyingine tena katika sherehe hizi wafanyakazi bora wametambuliwa na kupewa
tuzo. Mnastahili pongezi zetu sote kwa kufanya kazi kwa bidii, maarifa na
nidhamu na kutambuliwa. Wahenga walisema, ”Chanda
chema huvishwa pete”. Nawapongeza TUCTA na waajiri kwa kutambua umuhimu wa
kutoa tuzo kwa wafanyakazi bora. Inaongeza ari ya kufanya kazi na tija kazini.
Tafadhali udumisheni utaratibu huu. Kwa
wale ambao hawakupata safari hii wasikate tamaa na wao siku yao yaja waongeze
bidii, maarifa na nidhamu kazini ili mwakani, siku kama ya leo iwe zamu yao
kupongezwa.
Risala ya Wafanyakazi
Ndugu Kaimu Rais wa TUCTA,
Wafanyakazi Wenzangu,
Nimeisikiliza
kwa makini sana risala yenu iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa TUCTA Ndugu
Nicholas Mgaya ambaye anastahili pongezi kwa kuwasilisha vizuri na kueleweka.
Ni risala nzuri iliyosheheni mawazo mazuri ya kujenga. Ndani yake inayo maombi,
lakini pia mapendekezo. Napenda kuwahakikishia kuwa mapendekezo yote nimeyachukua
na tutakwenda kuyafanyia kazi. Baadhi ya maombi si mapya, yamerudiwa ili kuweka
msisitizo. Mengine majawabu yake tunayo,
nitayatolea maelezo katika hotuba yangu.
Kauli Mbiu
Wafanyakazi Wenzangu,
Nawapongeza kwa Kauli mbiu yenu isemayo, ”Utawala Bora Utumike Kuondoa Kero za
Wafanyakazi”. Kauli mbiu hii ni
muafaka na maridhawa kabisa. Ni ukweli
usiopingika kuwa utawala bora ni jambo muhimu sana na pale ambapo upo si tu kwamba husaidia kutatua kero za
wafanyakazi, bali pia huepusha mikwaruzano na migogoro kati ya wafanyakazi na
waajiri.
Wafanyakazi Wenzangu,
Uzoefu
unaonyesha kuwa migogoro ya wafanyakazi na waajiri hujitokeza zaidi pale ambapo
kanuni za utawala bora za ushirikishwaji, uwajibikaji na uwazi hazifuatwi.
Usiri usiyo wa lazima katika uamuzi, hufanya hata uamuzi mzuri kutiliwa shaka
na kujenga hofu isiyostahili kuwepo. Wakati mwingine inaweza kusababisha hata uamuzi
mzuri kukataliwa. Pia, ukosefu wa
taarifa sahihi unaweza kusababisha wafanyakazi kutoa madai yasiyotekelezeka kwa
sababu ya kuwa na matarajio makubwa mno kuliko uwezo wa mwajiri kumudu.
Tumejifunza,
vilevile, kuwa utawala bora hauishii kwenye kutunga sheria na kuunda taasisi na
vyombo vya usimamiaji na utekelezaji wa Sheria. Utawala bora hauna budi kuwa sehemu
kamili ya utamaduni wa kazi na uhusiano ambao unapaswa kuzingatiwa na waajiri
na waajiriwa. Wakati mwajiri anawajibika kuwa muwazi kwa wafanyakazi wake na
kuwatimizia stahili zao kama inavyopasika, waajiriwa nao wanawajibika kumtendea
haki mwajiri kwa kufanya kazi kwa bidii na kuheshimu taratibu za kazi ikiwa ni
pamoja na zile zihusuzo namna ya kuwasilisha madai yao.
Waajiri na
waajiriwa kudai haki zao hakuwaondolei wajibu wao kwa kila mmoja wao. Hivyo basi, kudumisha utawala bora kunawataka
waajiri na wafanyakazi kuheshimu Sheria za nchi zikiwemo zile zinazotawala uhusiano
na ajira sehemu za kazi. Hapa
nazungumzia, Sheria ya Majadiliano katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2003 na
Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya Mwaka 2004.
Ndugu Zangu;
Lazima tutambue na kukubali kuwa ufanisi sehemu za kazi
hutegemea uhusiano uliopo baina ya wafanyakazi na waajiri. Kama umejengwa juu
ya misingi ya kuheshimu sheria na majadiliano, mambo huwa mazuri. Vitisho vya mwajiri na migomo ya
wafanyakazi si suluhisho la kuondoa kero
za wafanyakazi. Kwa jumla hupunguza
ufanisi. Hivyo basi, lazima tufanye kila
tuwezalo kujenga uhusiano mwema kati ya waajiri na waajiriwa. Ni kichocheo kikubwa cha watu kufanya kazi kwa
bidii, kuongeza tija na uzalishaji sehemu za kazi hivyo kumwongezea mwajiri kipato
na uwezo wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
Hali ya Uchumi
Ndugu Viongozi na Ndugu Wafanyakazi;
Mwenendo wa
uchumi wetu katika mwaka 2013/2014 ni mzuri.
Uchumi umeendelea kuimarika ikilinganishwa na mwaka uliopita. Ukuaji wa
uchumi unategemewa kuongezeka kutoka asilimia 7.0 ya mwaka 2013 hadi asilimia 7.2 mwaka huu. Haya ni matunda ya kazi nzuri ya wafanyakazi, wakulima
na wadau wengine nchini. Tunayo kila
sababu ya kujipongeza kwa mafanikio haya.
Habari nyingine
njema kwa wafanyakazi ni kwamba mfumuko wa bei umeteremka kutoka asilimia 9 tulipokutana mwaka jana hadi
asilimia 6.3 tunapokutana leo. Azma yetu ni kutaka ubaki chini ya asilimia 10 na hasa uwe asilimia 5
au chini ya hapo ifikapo Juni, 2015. Tunahangaikia
sana kushuka kwa mfumuko wa bei kwa vile unapokua juu, unasababisha hali ngumu
ya maisha kwa wafanyakazi. Tukidhibiti
mfumuko wa bei uongezaji wa viwango vya mishahara utakuwa na tija. Aidha, inamuwezesha hata yule mwenye mshahara
mdogo kuweza kukidhi baadhi ya mahitaji yake muhimu, hivyo kumpunguzia ukali wa
maisha. Kwa sababu hiyo, hatuna budi
kuongeza bidii katika kukuza uchumi na kushusha mfumuko wa bei. Kwa vile hapa tulipofika sio ukomo wa uwezo
wetu, naamini tunaweza kupata mafanikio makubwa zaidi tukiongeza utawala bora
mahala pa kazi. Kiwango cha ukuaji wa
uchumi kinaweza kuwa kikubwa zaidi na kutunufaisha sote.
Mabaraza ya Wafanyakazi
Ndugu Wafanyakazi;
Hatuwezi
kuzungumzia utawala bora mahala pa kazi bila ya kuwa na ushirikishwaji wa
wafanyakazi. Ushirikishwaji wa wafanyakazi, unawezekana tu pale ambapo yapo mabaraza
ya kazi na yanafanya kazi. Mabaraza ya kazi ni fursa kwa wafanyakazi kuwakilisha
na kujenga madaraja kati ya menejimenti na
wafanyakazi. Madaraja haya hujenga mazingira ya kuwezesha madai ya wafanyakazi
kufika katika menejimenti, na uamuzi kufanywa na mrejesho wa menejimenti
kuwafikia wafanyakazi.
Nimepata
taarifa isiyofurahisha kuwa bado zipo taasisi chache za Serikali ambazo hazijaunda
mabaraza hayo. Nimeambiwa pia kwamba baadhi ya yale mabaraza yaliyoundwa
hayakutani kama inavyopasa. Hata hawakutani kujadili bajeti za taasisi zao,
jambo ambalo ni sharti la msingi kutekelezwa kwa kisingizio cha kukosa fedha. Madai haya hayaingii akilini hata kidogo. Mbona semina na vikao vya menejimenti vyenye
posho nono hatuoni vikiachwa kufanyika?.
Napenda kuwakumbusha
wakuu wa taasisi zote za umma kuwa uundwaji mabaraza ya wafanyakazi na
ushirikishwaji wa mabaraza hayo katika mchakato wa Bajeti sio jambo la hiari
bali ni matakwa ya kisheria. Wasiounda mabaraza na wale wasioitisha vikao vya
mabaraza kujadili bajeti za taasisi zao wanavunja sheria. Hili ni jambo
lisilovumilika. Nimewaagiza Waziri wa Kazi na Ajira na Katibu Mkuu Kiongozi
wahakikishe kuwa Wizara zote na taasisi zote za umma zinazingatia Agizo la Rais Na. 1 la Mwaka 1970 pamoja na matakwa ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na.6 ya
Mwaka 2004. Lazima wahakikishe kuwa mabaraza yanaundwa mapema iwezekanavyo, na
zile Wizara, Idara na Taasisi zisizoitisha mabaraza yao zibanwe kufanya hivyo
bila ajizi.
Umuhimu wa Vyama vya Wafanyakazi Mahali pa Kazi
Ndugu Wafanyakazi;
Jambo
lingine ambalo limenisikitisha sana ni taarifa kuwa bado wapo waajiri hasa
katika sekta binafsi ambao wanakaidi matakwa ya kisheria ya kuwepo kwa matawi
ya vyama vya wafanyakazi mahala pa kazi. Naambiwa hata pale wafanyakazi
wanapoanzisha mabaraza hayo, wale wafanyakazi wanaokuwa mstari wa mbele kudai
kuwepo matawi hayo au kutetea haki za wafanyakazi wamekuwa wanapata wakati
mgumu. Huishia kuhamishwa au hata kufukuzwa
kazi. Aidha, wapo baadhi ya waajiri ambao wameanzisha mifumo mbadala ambayo
haiko kisheria katika kukwepa kushughulikia maslahi ya wafanyakazi.
Napenda
kurudia na kusisitiza kuwa kuwepo kwa matawi ya vyama vya wafanyakazi mahala pa
kazi si suala la hiyari bali ni matakwa ya kisheria. Hivyo, hakuna sekta,
kampuni wala mwekezaji ambaye yuko juu ya sheria hii. Ni vizui ukaeleweka kuwa hii
si tu ni sheria ya nchi yetu peke yake, bali ni matokeo ya mikataba ya
kimataifa na ni haki ya msingi ya wafanyakazi na utawala bora.
Ndugu Viongozi na Ndugu
Wafanyakazi;
Sisi katika
Serikali ni mashahidi wa manufaa ya kuwepo kwa matawi ya wafanyakazi mahala pa
kazi. Uzoefu wetu umetuthibitishia kuwa pale ambapo kuna matawi ya vyama vya
wafanyakazi ambayo yanatimiza majukumu yake vizuri na menejimenti inatimiza
wajibu wake ipasavyo uhusiano wa kikazi huwa mzuri. Inasaidia kupunguza migogoro,
kuepusha migomo na huongeza tija na ufanisi. Matawi hayo hutoa fursa ya
majadiliano na mazungumzo kati ya wafanyakazi na waajiri. Si kweli hata kidogo kuwa, kuwepo kwa matawi
haya hukwamisha ufanisi mahala pa kazi.
Nimemwagiza
Waziri wa Kazi kuhakikisha kuwa matawi ya vyama vya wafanyakazi yanakuwepo
mahala pa kazi. Pia, ahakikishe kuwa wakaguzi wanapita sehemu za kazi na
kukagua utekelezaji wa sheria kuhusu kuwepo kwa matawi hayo. Wale waajiri
wanaokaidi wachukuliwe hatua za kisheria bila kuoneana muhali. Aidha, nimemtaka
asisite kuwachukulia hatua zipasazo za kinidhamu, wakaguzi wanaoshirikiana na
waajiri kudhoofisha haki za wafanyakazi. Hawa ni watu walioshindwa kutimiza
majukumu yao hivyo wasivumiliwe.
Wanaipaka matope Serikali.
Wapo Wakaguzi ambao wanakwazwa na kukaa kituo
kimoja kwa muda mrefu, wamezoeleka mno na wamejenga mazoea yasiyofaa kati yao
na waajiri na wanashirikiana kuwakandamiza wafanyakazi. Wahamishwe. Wakati huohuo wakumbusheni kuwa kazi yao ni
kusimamia sheria, kutetea haki za wafanyakazi na waajiri na kamwe sio kuwa
mawakala wa kuwasaidia waajiri kukiuka sheria.
Hatua za Serikali dhidi ya Uwakala wa Ajira
Ndugu Wafanyakazi;
Nimefurahishwa sana na uamuzi wa Mheshimiwa Gaudensia
Kabaka, Waziri wa Kazi na Ajira na viongozi wenzake Wizarani wa kufuta mfumo
mpya ulioanzishwa wa makampuni kuajiri kupitia uwakala wa ajira. Naunga mkono uamuzi wenu wa kupiga marufuku utaratibu
unaofanywa na baadhi ya Wakala Binafsi
wa Huduma za Ajira nchini wa kukodisha
wafanyakazi katika Makampuni. Utaratibu huu ni kinyume cha Sheria ya
Huduma za Ajira Na. 9 ya 1999. Sheria ya
Huduma ya Ajira inaelezea majukumu ya msingi ya Wakala Binafsi wa Huduma za
Ajira kuwa ni kuwaunganisha watafuta
kazi na waajiri na siyo wao kuwa waajiri na kukodisha wafanyakazi kwa makampuni.
Wakala wa Ajira
kufanya mambo kinyume na matakwa ya sheria haikubaliki. Anawakosesha wafanyakazi haki zao za msingi kama vile mishahara,
huduma za hifadhi ya jamii, likizo ya uzazi, matibabu, mafunzo na mengineyo. Inaondoa
uwajibikaji wa moja kwa moja wa waajiri kwa
wafanyakazi wao. Hili ni jambo ambalo hatuwezi kuliacha liendelee. Nimempa
Waziri wa Kazi na Ajira baraka zangu
zote kulishughulikia kwa nguvu zake zote na kwa umakini na ufanisi mkubwa ili tuweze
kukomesha kabisa dhulma hii.
Uimarishaji wa Vyombo vya Mashauriano
Wafanyakazi wenzangu;
Jambo lingine ambalo linahitaji kupatiwa ufumbuzi katika
kuimarisha uhusiano kati ya wafanyakazi na waajiri ni ufanisi wa vyombo vya
mashauriano. Serikali imefanya kazi nzuri ya kuunda vyombo hivi ikiwemo Baraza
la Mashauriano (LESCO). Lengo la kuunda mabaraza hayo ni kutoa fursa ya usuluhishi
wa migogoro ya kikazi na maslahi ya wafanyakazi kabla ya kuiwasilisha katika
mifumo ya kimahakama.
Pamoja na nia njema ya Serikali, chombo hiki kimeendelea
kulalamikiwa kwamba hakitekelezi wajibu wake kwa ukamilifu. Mashauri
yanayowasilishwa hayatatuliwi kwa wakati kutokana na Baraza hili kutoitisha
vikao, kwa madai ya ufinyu wa bajeti. Matokeo yake, wafanyakazi aidha wanaamua
kufikisha migogoro yao kwa Waziri wa Kazi, au kwenda mahakamani au kuchukua
sheria mkononi. Hatua zote hizi nje ya
matumizi ya Baraza la LESCO, si endelevu na hazijengi mazingira ya maridhiano
kati ya waajiri na wafanyakazi. Kwa
jumla zinadhoofisha utawala bora.
Nimeelekeza, kuanzia bajeti
ya mwaka wa fedha 2014/2015, Wizara
ihakikishe inatenga fedha za kutosha za kuwezesha Baraza la LESCO kufanya vikao
vyake. Aidha, bajeti hiyo ilindwe ili kuhakikisha kuwa pesa hizo zinatumika kwa
ajili ya kazi za Baraza la Mashauriano.
Ni jambo linalowezekana. Nataka
tuone kuwa kuanzia mwaka ujao wa fedha Baraza hili linafanya kazi yake ipasavyo. Sote tunakubaliana kuhusu umuhimu wake kuwa ni
mkubwa na ipo mifano ya nchi nyingine
ambazo Baraza hili hufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Naamini kwamba, kwa kuwa changamoto yetu si udhaifu wa
Sheria yenyewe iliyounda LESCO bali ufanisi katika utendaji tu, upatikanaji wa
fedha za kutosha utawezesha Baraza hili kufanya kazi kwa ufanisi. Mwisho wa
yote tutaepusha migogoro isiyo ya lazima, lakini pia tutaimarisha utawala bora
kwa kujenga madaraja kati ya watumishi na waajiri pale panapojitokeza
mikwaruzano.
Ushiriki wa Wafanyakazi
kwenye Bodi za Mashirika
Wafanyakazi Wenzangu,
Sambamba na
kulihuisha Baraza la LESCO, Serikali inalifanyia kazi suala la kushirikisha wafanyakazi
katika Bodi za Mashirika ya Umma. Tunafanya hivyo kwa kutambua kuwa, Bodi za
Mashirika ni vyombo muhimu vinavyofanya uamuzi wa kisera na kiuendeshaji wa
mashirika. Uamuzi wake hugusa moja kwa
moja maslahi ya wafanyakazi hivyo uwakilishi wao ni muhimu.
Natambua
kuwa tayari yapo mashirika ambayo kwa mujibu wa Sheria ya kuanzishwa kwake,
yametambua uwakilishi wa wafanyakazi katika Bodi zake. Lakini yapo mashirika
mengine hayana sharti hilo katika Sheria zilizounda mashirika hayo. Manufaa na
umuhimu wa kuwashirikisha wafanyakazi si mambo yanahotaji mjadala. Yapo
wazi. Katika yale mashirika ambayo Bodi
zake zina wajumbe kutoka vyama vya wafanyakazi, tumeona namna ambavyo mchango
wa wafanyakazi umekuwa wa msaada mkubwa.
Nimeelekeza
Wizara husika na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuchukua hatua za haraka kuandaa
na kuwasilisha muswada wa Sheria Bungeni wa kulirasimisha jambo hili kwa
mashirika yote ya umma. Lengo letu ni kutaka kuhakikisha kuwa, jambo hili
muhimu haliwi suala la utashi tu wa Shirika husika, bali ni utaratibu rasmi wa
kisheria. Naamini ushiriki wa wafanyakazi katika Bodi za Mashirika utaimarisha utawala
bora na kupunguza kero za wafanyakazi mahala pa kazi.
Maslahi ya Wafanyakazi
Ndugu Kaimu Rais, Ndugu
Viongozi na Ndugu Wafanyakazi;
Nafahamu kuwa
hotuba yangu haitakuwa imekamilika bila kuzungumzia maslahi ya wafanyakazi. Na,
wengi hasa wanasubiri kusikia nasema nini kuhusu nyongeza ya kima cha chini cha
mshahara na kupungua kwa kodi ya mapato, yaani Paye As You Earn (P.A.Y.E).
Napenda
kurudia kuwahakikishia kuwa mimi na wenzangu Serikalini hatuna upungufu wa
dhamira ya kufanya hivyo. Tumethibitisha hivyo miaka iliyopita na tutaendelea
kuwa hivyo. Leo nitapenda kuzungumzia mambo
matatu: La kwanza ni kuhusu Kima cha Chini cha Mshahara. Kama tulivyoahidi mwaka jana, Serikali
ilipandisha kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa Umma kwa asilimia 41. Kwa ongezeko hilo, kima
cha chini cha watumishi wa umma kiliongezeka kutoka shilingi 170,000 hadi shilingi
240,000. Na mwaka huu nawaahidi tena
kuwa tutaongeza. Najua kwamba nyongeza
hii si kubwa kuliko vile ambavyo wafanyakazi na hata mimi ningependelea iwe. Kwa kweli kinachotukwaza ni mapato ya
Serikali kutokuwa makubwa kumudu nyongeza kubwa ya mshahara kwa wakati. Nyongeza hii peke yake inaifanya Serikali
kutumia asilimia 44.9 ya bajeti ya
Serikali kulipa mishahara na asilimia 10
ya pato la taifa (GDP). Kwa vigezo vyo vyote vile kiwango hiki ni kikubwa mno
hivyo ni kielelezo thabiti cha dhamira yetu njema na kujali.
Isitoshe naomba
mkumbuke kuwa mwaka 2005 kima cha chini cha mshahara kilikuwa shilingi 65,000.00. Hivyo ndani ya miaka saba tumeongeza kima cha chini karibu mara nne
ya ilivyokuwa na kufikia kima cha chini cha sasa. Nawaahidi mwaka huu tutaongeza tena. Kama nilivyogusia, hatuwezi kutoa nyongeza
kubwa mara moja lakini, kidogo kidogo tunaweza. Na tumeweza. Naamini, miaka mitano ijayo mambo yatakuwa
mazuri zaidi wakati mapato ya Serikali yatakapoongezeka sana mauzo ya gesi
asilia yatakapoanza.
La pili ni Kima cha Mishahara
Katika Sekta Binafsi: Kima cha chini cha m
ishahara katika sekta binafsi bado
hakinifurahishi. Kwa upande wa sekta binafsi, mfumo wa upangaji wa kima cha
chini cha mshahara unatawaliwa na Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7 ya Mwaka
2004. Sheria hii inaanzisha Bodi za Mishahara za kisekta ambazo zina wajibu wa
kutoa mapendekezo kwa Waziri wa Kazi na Ajira kuhusu kima cha chini cha mshahara katika sekta husika. Naambiwa
kuwa Bodi hizi zinapata changamoto katika utekelezaji wa majukumu yake kwa kuwa
waajiri hawatoi ushirikiano wa kutosha.
Mnamo mwezi Juni,
2013, Mhe. Waziri wa Kazi na Ajira alitangaza mishahara ya kima cha chini
kisekta kupitia Gazeti la Serikali Na. 196/2013
kwa sekta 12 za Madini, Afya, Kilimo, Nishati, Usafirishaji, Viwanda,
Ujenzi, Ulinzi binafsi, Shule binafsi, Hoteli, Huduma za Majumbani na
Mawasiliano. Taarifa ninayopata ni kuwa, sehemu kubwa ya waajiri wa sekta
binafsi hawazingatii viwango hivyo.
Nimemuelekeza Waziri wa Kazi awabane wsiotekeleza watekeleze Tuzo
alizotoa.
Naguswa sana na kilio cha wafanyakazi katika sekta
binafsi. Sisi kama Serikali hatuwezi kukwepa wajibu wa kuwasaidia. Nimeelekeza
kuwepo na mkakati maalum kushughulikia jambo hili. Katika mkakati huo, nashauri utaratibu wa Utatu
yaani Wafanyakazi, Waajiri na Serikali utumike kufanya tathmini na kubaini
matatizo yaliyopo na kupendekeza namna bora ya kuhakikisha wafanyakazi wa sekta
binafsi wanapata mishahara wanayostahili. Katika mkakati wa muda mrefu,
tumekubaliana na viongozi wenu kuimarisha vyombo vya mashauriano, usimamizi na
bodi za kisekta ili huko mbele ya safari visimamie kwa ukamilifu jambo hili.
Jambo la tatu ni Kodi ya Mapato
kwa wafanyakazi yaani PAYE: Kumekuwepo pia na ombi la muda mrefu la kupunguza kodi
inayokatwa kwenye mishahara ya wafanyakazi kuwa chini ya asilimia 10. Kama
nilivyoahidi mwaka jana, hili tutaendelea kulishughulikia kadri uwezo wa
Serikali utakaporuhusu. Tumeshafanya hivyo kabla, na hatuna sababu ya kutofanya
hivyo huko tuendako. Tayari tumepunguza
kutoka asilimia 18.5 mwaka 2007 hadi
asilimia 13 hivi sasa. Maombi yenu tumeyapokea, tuachieni, tuangalie
nini tunachoweza kufanya kama miaka iliyopita.
Kwa jumla ni nia yetu kuendelea kufanya hivyo mwaka hadi mwaka,
tunakwazwa na uwezo mdogo wa mapato ya Serikali.
Mageuzi katika Mifuko ya Kijamii
Wafanyakazi wenzangu;
Kama
nilivyosema wakati wa sherehe za Mei Mosi zilizofanyika mkoani Mbeya mwaka
jana, Serikali ina dhamira ya dhati ya kupanua wigo wa hifadhi ya jamii kwa
wafanyakazi na kwa wananchi wote kwa
ujumla. Hatua kwa hatua tutaendelea kufanya marekebisho katika Hifadhi ya Jamii
nchini ili iweze kukidhi haja hiyo.
Eneo moja
ambalo tumejiandaa kulitekeleza kuanzia Julai, 2014 ni kuhusu fidia kwa
wafanyakazi wanaoumia au kuathirika wakiwa kazini. Wote tunafahamu kwamba tangu
mwaka 2008 Serikali ilipitisha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Na. 20 ambayo inaunda
Mfuko wa Fidia utakaoshughulikia malipo yaliyo bora zaidi ya fidia kwa
wafanyakazi wanaoumia au kufariki au kupata maradhi yatokanayo na kazi kuliko
ilivyo sasa. Mfuko huu utahudumia
wafanyakazi wa sekta zote yaani sekta binafsi na ya umma na utatoa mafao bora
zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.
Tunafanya
hivyo kutokana na uzoefu tulioupata wa wafanyakazi wengi hasa katika sekta binafsi
kushindwa kupata fidia stahili, wakati mwingine kutokana na uchanga wa waajiri
wao. Kwa kuwa na mfuko huu kutawapunguzia waajiri mzigo wa kuwalipa fidia
wafanyakazi wao hasa wakati ambao hawana uwezo wa kufanya hivyo. Mfuko utawapa wafanyakazi uhakika wa kulipwa
fidia yao pale watakapopata madhara mahala pa kazi. Serikali itachangia asilimia moja ya jumla ya mishahara ya
wafanyakazi kila mwezi kuanzia mwezi Julai, 2014. Waajiri binafsi nao watachangia asilimia 0.5 ya jumla ya mishahara ya
wafanyakazi wao.
Wafanyakazi Wenzangu;
Eneo jingine ambalo tuliahidi kulifanyia kazi
ni kuhusu kuainisha mafao ya pensheni. Mchakato huu unaendelea vizuri na
nafahamu kuwa Mamlaka ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na Wadau yaani Vyama
vya Wafanyakazi wanatarajiwa kukutana tarehe 5 Mei, 2014 kwa majadiliano zaidi.
Kikao hicho kitajadili ulingano wa
mafao yanayotolewa na Mifuko ya Hifadhi
ya Jamii kwa kuweka vikokotoo bora vya Mafao ya Pensheni.
Ni vizuri
kukumbushana kwamba, kuwa na vikokotoo vizuri ni jambo moja, na kuhakikisha
uendelevu wa mifuko ya hifadhi ya jamii ni suala lingine. Hivyo, wakati
tunaendelea na majadiliano hayo, hatuna budi pia kutoa umuhimu katika kuelimishana juu ya
umuhimu na wajibu wa waajiri kuwasilisha michango ya wanachama. Mifuko ya hifadhi ya jamii inatakiwa kuhakikisha
kuwa inakusanya michango ya wanachama wake na kuwekeza kwa umakini mkubwa. Wanachama wao wanatakiwa kuhakikisha kuwa michango
yao inabaki katika mifuko ya hifadhi ya jamii ili ije kuwafaa wakati wa shida
na maisha ya uzeeni, badala ya tabia ya sasa ya watumishi kuamua kushirikiana
na waajiri kutokatwa michango hiyo, au kujitoa katika mifuko hiyo kila
wanapobadilisha ajira kutoka kwa mwajiri mmoja kwenda kwa mwajiri mwingine.
Madai ya Waalimu
Wafanyakazi Wenzangu,
Serikali pia imeendelea kushughulikia madai mbalimbali
ya watumishi wa umma hususan madeni ya mishahara na yasiyokuwa ya
mishahara. Tumekamilisha uhakiki wa
madeni kwa wafanyakazi wasiokuwa walimu.
Hazina wameniarifu kuwa yatalipwa kabla ya mwaka ujao wa fedha. Kwa upande wa walimu, Serikali kwa kushirikiana
na Chama cha Walimu (CWT) tumekuwa tunafanya uhakiki wa madeni ya walimu katika
Halmashauri zote 147 za Tanzania Bara.
Kazi imekamilika kwa Halmashauri 96 na inaendelea kwa Halmashauri 51
zilizosalia. Nimeambiwa kuwa madeni
yaliyohakikiwa yameanza kulipwa. Na,
kama nilivyosema kwa wafanyakazi wasiokuwa walimu ni makusudio ya Hazina kuwa
madeni hayo yalipwe katika mwaka huu wa fedha.
Ni
jambo la kutia faraja kwamba, katika kufanya kazi ya uhakiki wa madeni ya
walimu. Serikali na Chama cha Walimu tumeweza
kubaini mzizi wa fitina. Tumekubaliana kuutafutia dawa ya kuung’oa ili tatizo
hili lisijirudie.
Kwa ajili hiyo, nimeelekeza Wizara na Taasisi
zinazohusika hasa Wizara ya Fedha, Wizara ya Elimu na Mafunzo na Ufundi na Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu maofisa
wa Serikali, wanaohusika na udanganyifu huu. Halikadhaika, wafanyakazi
walioghushi stakabadhi nao wachukuliwe hatua za kisheria. Kwa muda mrefu,
udanganyifu na hila za watumishi hawa zimechochea kutokuelewana na
kutokuaminiana kati ya walimu na Serikali.
Ifike mahala
sasa, walimu na Serikali tupate suluhu ya kudumu baada ya kumpata mchawi wetu.
Tumekubaliana kuendelea na mfumo huu wa uhakiki wa pamoja kama msingi wa
kutatua tatizo hili la muda mrefu. Huu ni mfano mzuri wa namna utawala bora
unavyoweza kutatua kero za wafanyakazi kupitia ushirikishaji na uwazi.
Kuhusu
muundo mpya wa Utumishi wa Walimu, habari njema ni kuwa muundo huo
umekwishapitishwa na unatarajiwa kuanza kutumika tarehe 1 Julai, 2014. Suala la upandishaji wa madaraja ya walimu nalo
linakwenda vizuri ambapo hadi kufikia Aprili 2014, walimu 30,236 walikuwa wamepandishwa vyeo.
Kuhusu
wimbo wenu, Shemeji mshahara mdogo.
Nimefuatilia nimebaini ni kweli kumekuwa na ucheleweshaji. Nimefuatilia Benki Kuu wanasema walitoa pesa
mapema, lakini kumekuwepo na mkwamo mahali ambapo tutapatafuta.
Utoaji Holela wa Vibali vya Ajira kwa Wageni
Ndugu Kaimu Rais wa TUCTA;
Wafanyakazi wenzangu,
Yamekuwepo
malalamiko kuwa kumekuwepo na utoaji holela wa vibali vya kazi kwa wageni
kufanya kazi nchini. Naambiwa siku hizi
hata zile ajira ambazo Watanzania wana
ujuzi nazo hujazwa na wageni. Serikali
imeyafanyia kazi malalamiko haya na kugundua kuwa udhaifu upo kwenye kuwepo kwa
taasisi zaidi ya moja inayoshughulika na utoaji wa vibali kwa wageni kuishi na
kufanya kazi nchini. Hali hii inatoa
mwanya kwa watu wasiokuwa waaminifu kutoa vibali kwa watu wasiostahili.
Serikali
imeamua kuzifanyia marekebisho sheria husika na iko mbioni kuwasilisha Bungeni
Muswada wa Sheria ya Vibali vya Ajira. Nimeelekeza kuwa jitihada zifanyike ili Muswada
huo uwasilishe kwenye kikao cha Bunge la Oktoba, 2014. Sheria hii sasa italiweka suala la vibali vya
kazi kushughuhulikiwa na taasisi moja na hivyo kuweka udhibiti katika utoaji wa
vibali hivyo.
Ndugu Wafanyakazi;
Niruhusuni
nichukue fursa hii, pia, kukumbusha kuhusu umuhimu wa wafanyakazi kuheshimu na
kuthamini kazi. Waswahili wana msemo “Usichezee kazi, chezea mshahara”. Yapo madai yanayojirudia kutoka kwa waajiri
kuwa wafanyakazi wa Kitanzania hawathamini na kuheshimu kazi zao. Wanatuhumiwa kwa uvivu, udokozi na nidhamu
ndogo. Napata taabu kukubali madai haya kuwa
hii ndio sifa ya wafanyakazi wote wa Kitanzania. Leo nimetunuku tuzo kwa wafanyakazi bora na tumekuwa
tunafanya hivyo kila mwaka. Kitendo hiki
ni ushahidi kuwa wafanyakazi hodari wapo.
Hata hivyo, siwezi kusema wavivu, wezi na watovu wa nidhamu hawapo. Lakini, sina uhakika na ukweli wa madai
yanayotoa sifa mbaya na kutia doa baya
kwa Wafanyakazi wa Kitanzania.
Sifa hizo hasi ndizo zinazowashawishi waajiri
na hasa wawekezaji kutafuta wafanyakazi nje.
Ninawaomba viongozi na wanachama wa vyama vya wafanyakazi mlitafakari
suala hili kwa uzito unaostahili kwani linaelekea kuaminika. Kulikataa tatizo peke yake hakutoshi kwani hakutatui
tatizo lililopo, zaidi ya kutupa faraja ya muda tu. Natoa rai kwa vyama vya wafanyakazi na Wizara
ya Kazi na Ajira kulifanyia kazi jambo hili haraka.
Mchakato wa Katiba
Wafanyakazi Wenzangu,
Katika
sherehe za Mei Mosi zilizofanyika mwaka jana kule Mbeya, mlitoa rai ya
wafanyakazi kushirikishwa katika mchakato wa kutunga Katiba Mpya. Niliwaahidi kuwa mtashirikishwa kwa vile wafanyakazi
ni sehemu kubwa sana ya jamii yetu na kundi muhimu sana katika taifa. Nimetimiza ahadi yangu wakati wa kuteua Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na Wajumbe 201 wa Bunge Maalum la Katiba. Kuna uwakilishi mkubwa wa wafanyakazi na
kumfanya Ndugu Maige, Mwenyekiti wa ATE alalamikie uwakilishi mdogo wa waajiri. Kazi yangu nimemaliza, sasa iko kwa
wawakilishi wenu kutumia vizuri fursa waliyopata kupigania haki na maslahi ya wafanyakazi
bila ya kusahau maslahi ya Watanzania wengine.
Bahati nzuri wajumbe wengi ni wafanyakazi hata kama hawakuingia Bungeni
wakiwa moja kwa moja wanawakilisha wafanyakazi. Kwa hiyo ni rahisi kwa masuala ya wafanyakazi
kutetewa. Hamna budi kuwasiliana nao.
Jambo
muhimu kwenu kufanya ni kujipanga vizuri kwa hoja za kuwapa wawakilishi wenu
kuzipigania. Msipofanya hivyo mtakuja
kujikuta wawakilishi wenu wakatekwa na makundi yenye agenda na misimamo
isiyoendeleza maslahi yenu. Sisemi wasijihusishe
na mambo mengine yenye maslahi kwa taifa, la hasha!. Ninachosema wasifanye hayo na kuacha kusemea
yenye maslahi ya wafanyakazi. Wanaweza
kukosekana watu wa kuyasemea mkajutia fursa hii.
Naungana
nanyi kusikitika kutokana na mienendo na kauli zisizoridhisha za baadhi ya
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Naungana nanyi pia kuwasihi watumie lugha ya
staha na wazo la kutafuta majawabu kwa njia ya mashauriano itatuwezesha kumaliza
tofauti za kambi. Nawasihi waliotoka
Bungeni warejee pale Bunge Maalum la Katiba litakapoanza upya baada ya
mapumziko ya kupisha Bunge la Jamhuri na Baraza la Wawakilishi kufanya shughuli
za lazima hususan bajeti za Serikali zetu mbili.
Hitimisho
Ndugu Kaimu Rais wa TUCTA,
Katibu Mkuu na Wafanyakazi Wenzangu;
Naomba
nimalize kwa kurudia kuwashukuru tena kwa kunipa nafasi hii adhimu ya kujumuika
nanyi tena katika sherehe za mwaka huu. Napenda
kuwahakikishia, kwa mara nyingine tena, kwamba dhamira yangu binafsi, na ile ya
Serikali ninayoiongoza ya kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi iko
palepale. Kilio chenu ni kilio changu. Tumejitahidi katika kipindi hiki kutatua
matatizo ya wafanyakazi na mafanikio yake mnayaona. Nina imani kuwa tukishirikiana katika mwaka
mmoja uliobakia tutaweza kutatua kero nyingi zaidi.
Mwisho, napenda
kuwakumbusha kuwa, maslahi mazuri kwa wafanyakazi yana uhusiano wa moja kwa moja
na kuongezeka kwa tija, uzalishaji, na pato la waajiri katika sekta binafsi na sekta za umma.
Shime nawasihi muongeze juhudi ili nanyi mnufaike zaidi. Kwa upande wangu naamini kwamba neema haiko
mbali sana. Tumefanikiwa kuweka misingi
mizuri ya kiuchumi, tumeunda taasisi na kuweka mazingira mazuri ya kisheria na
kisera. Bahati nzuri Mwenyezi Mungu
ametushushia neema ya rasilimali ikiwemo gesi asilia. Vyote hivi kwa pamoja,
vinatupa matumaini kuwa ndoto yetu ya kufikia nchi ya uchumi wa kati mwaka 2025
itatimia. Inawezekana Timiza Wajibu Wako.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu
Ibariki Tanzania!
Asanteni
sana kwa kunisikiliza. Nawatakia sherehe njema.
No comments:
Post a Comment