MHESHIMIWA, Gaudentia Kabaka, Waziri wa Kazi na Ajira;
Mheshimiwa Daktari Makongoro Mahanga, Naibu
Waziri wa Kazi na Ajira;
Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Naibu Waziri –
TAMISEMI;
Mheshimiwa Magesa Mulongo, Mkuu wa Mkoa wa
Arusha;
Waheshimiwa Wabunge;
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini NSSF, Ndg,
Abubakar S. Rajabu;
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Ndugu
Crecentius Magori;
Menejimenti ya NSSF;
Wageni waalikwa wenzangu;
Ndugu Wadau wa Hifadhi ya Jamii;
Mabibi na Mabwana;
Shukrani na Pongezi
Nakushukuru Mheshimiwa Waziri na Mwenyekiti
wa Bodi ya Wadhamini wa NSSF kwa kunikaribisha kufungua mkutano wa nne wa wadau wa Hifadhi ya Jamii unaoanza
leo hii hapa jijini Arusha. Mkutano wa mwaka huu una umuhimu wa kipekee kwani
ni fursa ya kujipongeza kwa NSSF kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka
1964. Wakati ule ikijulikana kama Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi (NPF).
Nakupongeza
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini na wajumbe wako, Mkurugenzi Mkuu na Menejimenti
ya shirika pamoja na wafanyakazi wote wa NSSF kwa kazi nzuri mnayoifanya na
mafanikio yaliyopatikana. Kazi yenu inaonekana
na inapimika. Kutokana na kazi yenu nzuri, mnawatia moyo wanachama wenu na
kuwapa imani kuwa amana zao walizowekeza kwenu ziko salama, na kwamba mko
tayari kukabiliana na changamoto za leo, na za miaka 50 ijayo.
Umuhimu wa Mikutano ya Wadau
Mheshimiwa Waziri na Wadau;
Nimefurahishwa na utamaduni wenu wa kuwa na mikutano
hii ya wadau kila mwaka. Ni utamaduni mzuri kwani unatoa fursa ya wadau
kushiriki katika kufanya tathmini ya mwaka hadi mwaka na kupeana mrejesho wa
hali ilivyo miongoni mwa wadau. Utaratibu huu unasaidia kuamsha ari ya kutekeleza malengo. Ni fursa
nzuri pia ya kuhuisha malengo yenu kuendana na mabadiliko ya mazingira, maana
tofauti na zamani, mabadiliko katika dunia ya sasa yanakwenda kwa kasi kubwa.
Huu ni utamaduni ambao hamna budi kuudumisha na kuuendeleza.
Umuhimu wa Hifadhi ya Jamii
Mheshimiwa Waziri na wadau wa hifadhi ya
jamii,
Hifadhi ya Jamii ni haki ya msingi na
asili ya kila mwanadamu. Msingi wa haki yenyewe ni kulinda thamani ya utu wa
binadamu. Haki hii inazingatia kuwa binadamu kwa asili ni mwanajamii, anastawi
tu akiwa miongoni mwa jamii na anachangia katika maendeleo ya jamii yake,
hivyo, anayo haki ya kusitiriwa na kupata hifadhi kutoka kwa jamii pale uwezo
wake wa kuchangia unapokoma kutokana na uzee, ulemavu au janga lisilotazamiwa.
Hifadhi ya jamii ina faida kwa
mwanajamii na jamii yenyewe. Kwa upande mmoja inamkinga mwanajamii dhidi ya
kupoteza utu na thamani katika jamii, na upande wa pili inaikinga na kuinusuru
jamii dhidi ya madhara ya kiuchumi na kiusalama yanayoweza kusababishwa na kuwa
na jamii iliyokata tamaa.
Upo uhusiano mkubwa kati ya ustawi wa jamii
na hifadhi ya jamii. Ndio maana, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Binadamu wa mwaka
1948 umetambua haki ya binadamu kupata hifadhi na Katiba ya nchi yetu ya mwaka
1977, nayo imetambua haki ya kupata hifadhi ya jamii. Katika Ibara ya 11, ibara
ndogo (i). Katiba inatamka kuwa “Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu unaofaa kwa ajili
ya kufanikisha utekelezaji wa haki ya mtu kufanya kazi, haki ya kupata
elimu na haki ya kupata msaada kutoka kwa jamii wakati wa uzee, maradhi
au hali ya ulemavu, na katika hali nyinginezo za mtu kuwa hajiwezi...” Huu ni wajibu wetu kikatiba
na tutaendelea kuutekeleza.
Hali ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii Nchini
Ndugu Wadau;
Shughuli za Hifadhi ya Jamii nchini imeanza miaka 50 iliyopita na hatua kubwa imepigwa
katika kipindi hicho. Sisi sote ni mashahidi wa mapinduzi makubwa yaliyofanyika katika Sekta
hii. Idadi ya mifuko, wigo wa wanachama
na idadi ya mafao.
Tulianza na Mfuko mmoja tu wa akiba ya wafanyakazi maaarufu kwa jina la NPF
mwaka 1964. Leo tuna mifuko 6 ya NSSF, PPF, LAPF, GEPF, PSPF na NHIF. Wigo wa wanachama
wa mifuko hii nao umetanuka. Mwanzoni ilihusu watumishi walioajiriwa, tena
walichaguliwa mfuko wa kujiunga nao kutokana na sekta zao lakini leo tunao
wanachama kutoka sekta binafsi waliojiajiri, na wako huru kuchagua mfuko wanaoupenda
kujiunga nao. Hali kadhalika, mafao yaliyokuwa yakitolewa wakati ule yalikuwa
ni mafao ya pensheni tu, tena kwa mkupuo mmoja, hivi sasa kuna mafao mengi na
malipo ni kwa mwezi katika uhai wote wa mwanachama. Mafao mengine hufaidisha
hata wategemezi wa mwanachama.
Mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya Hifadhi ya Jamii yamekuwa na
mchango mkubwa katika uchumi wa taifa letu. Sekta hii ilichangia wastani wa asilimia 11 ya pato la taifa kwa mwaka
2011/2012. Mtaji wa mifuko hii sasa umefikia shilingi trilioni 5,242 kutoka trilioni
1.36 mwaka 2005/2006. Kutokana na hali nzuri ya ukwasi tayari mifuko hii
imewekeza kiasi cha shilingi trilioni
4.4 mwaka 2012 ambapo asilimia 19 imewekezwa kwenye sekta ya
ujenzi na makazi, asilimia 18 kwenye
hisa na asilimia 63 kwenye amana za
serikali na mikopo.
Miaka 50 kutoka Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi
(NPF) hadi Mifuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)
Ndugu Wadau wa Hifadhi ya Jamii;
Serikali, kupitia Sheria Na. 28 ya
mwaka 1997, ilianzisha Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii – NSSF, kwa
kuboresha Shirika la Akiba ya Wafanyakazi (NPF) lililoanzishwa mwaka 1964. Maboresho hayo yalilenga kuongeza ubora na idadi ya
mafao, kupanua wigo wa wanachama na kuisaidia Serikali
katika kutoa huduma za hifadhi ya jamii. Mabadiliko haya yaliliwezesha Shirika
la NSSF kutoa mafao ya pensheni ya uzeeni, urithi na ulemavu kwa wanachama wake
pamoja na mafao mengine kama vile matibabu, uzazi, fidia ya kuumia kazini na
gharama za mazishi.
NSSF imeendelea kukua na kuimarika mwaka
hadi mwaka. Thamani ya mfuko imeongezeka kutoka shilingi trilioni 1.97 katika mwaka 2011/2012 hadi kufikia shilingi trilioni 2.24 mwaka 2012/2013. Kuongezeka huko kwa thamani ya mfuko
kumeambatana na kuongezeka kwa mafao yanayolipwa na NSSF kutoka shilingi bilioni 178 mwaka 2011/2012
hadi shilingi bilioni 228 mwaka 2012/2013.
NSSF imekuwa mchangiaji muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu kwa kuwekeza kwenye
miradi ya maendeleo inayochochea ukuaji wa uchumi na kuongezeka kwa ajira. Tumeona
manufaa ya uwekezaji wa NSSF katika ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, daraja la
Kigamboni, ujenzi wa Chuo Kikuu cha Nelson Mandela na miradi ya ujenzi wa
nyumba za watumishi wa umma na nyumba za wafanyakazi.
Inafurahisha kusikia kuwa shirika
limetunukiwa cheti cha kimataifa cha utoaji wa huduma bora (ISO 9001:2008
CERTIFICATION), na hivi karibuni, kutunukiwa cheti cha utawala bora kwa kufuata
kanuni bora za manunuzi na ugavi (PPRA Award). Kwa haya mawili nawapongeza sana
na kuwaomba muendelee na viwango hivi vya ueledi. Maana shirika lenu ni nyeti
katika uchumi wa taifa, kwa kuwa mmeaminiwa kuhifadhi na kuwekeza kwa fedha za
akiba za wanachama. Umakini mkubwa unahitajika katika kuwekeza. Hamna budi
kuwekeza vizuri ili mfuko uendelee kustawi na wanachama wake waendelee kupata
hifadhi kutoka kwenu.
Wajibu wa Serikali:
Usimamizi na Uendeshaji wa
Mifuko ya Hifadhi
ya Jamii
Ndugu Wadau wa Hifadhi ya Jamii;
Sisi katika Serikali tunao wajibu wa msingi
wa kulea mifuko hii ili iweze kustawi na
kuwa endelevu. Katika kutekeleza wajibu wetu huo, na kwa kuzingatia ukuaji wa
sekta yenyewe, Serikali ilianzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii (SSRA) mwaka 2010. Lengo kuu la
kuanzishwa kwa SSRA ni kusimamia na kuratibu shughuli zote katika Sekta ya
Hifadhi ya Jamii hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kufanya maboresho katika
nyanja za uwekezaji na mafao yanayotolewa kwa wanachama.
Naipongeza Wizara ya Kazi na Ajira pamoja
na Msimamizi na Mdhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwa kazi nzuri
wanayoifanya katika kusimamia mageuzi ya kiutendaji na ya uendeshaji wa Mifuko hii ya Hifadhi ya
Jamii. Naiomba SSRA iendelee kuboresha mazingira ya ushindani katika mifuko kwani
ushindani hatimaye huleta unafuu kwa wanachama. Tumeona namna ambavyo ushindani
umechochea kila Mfuko kuongeza ubunifu katika utoaji wa huduma na aina ya mafao
yanayotolewa. Kazi kubwa waliyonayo
sasa, ni kubuni mkokotoo mpya
utakaosaidia kuoanisha mafao yatolewayo na mifuko hiyo.
Wito kwa NSSF na
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
Ndugu wadau wa hifadhi ya jamii,
Pamoja na mchango mkubwa wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
katika uchumi na maendeleo ya taifa kwa ujumla, bado ni sehemu ndogo sana ya
Watanzania wanapata kinga dhidi ya majanga kupitia Mifuko hii. Takwimu
zinaonyesha kwamba kati ya Watanzania milioni
22.4 wenye uwezo wa kuzalisha kipato, waliomo katika Mifuko yote 6 si zaidi ya asilimia 6 tu. Idadi hii ni ndogo sana ukilinganisha na idadi ya
Watanzania ambao wanafanya kazi zenye kipato. Aidha idadi hii ni ndogo
ikilinganishwa na wastani wa asilimia 10
kwa nchi za Afrika na Kusini mwa Asia.
Kwa
mujibu wa tathmini ya Sekta ya Viwanda na Biashara Ndogondogo (SMEs) ya mwaka
2013, sekta isiyo rasmi ilichangia asilimia
39.7 ya pato la taifa kwa mwaka 2010. Vile vile, ilikadiriwa kuwa zipo SMEs
milioni 3 zinazoajiri wananchi milioni 5.2. Wito wangu kwenu ni mifuko
ya hifadhi ya jamii kutoka maofisini kwenda kuhamasisha wananchi wengi wajiunge
na mifuko hii. Waelezeni manufaa yake, na watoeni hofu zao juu ya fikra potofu
walizonazo kuhusu hifadhi ya jamii. Wengi wanaamini hifadhi ya jamii ni stahili
ya wafanyakazi wajiriwa tu, tena wafanyakazi wa kipato kikubwa. Wajulisheni
kuwa hivi sasa hifadhi ya jamii ni fursa huru kwa wote, wale walioajiriwa na
wale waliojiajiri. Wafafanulieni wale walio kwenye sekta isiyo rasmi kuwa,
utaratibu wa wao kujiunga, kuchangia na kunufaika. Waonyesheni mifano hai ya
wale wakulima na wajasiriamali namna wanavyochangia na wanavyofaidika.
Natoa rai
hii nikitambua kuwa wako wananchi wengi katika sekta ya kilimo na sekta isiyo
rasmi ambao kwa vipato vyao wangeweza kujiunga na hifadhi ya jamii. Nawapongeza
NSSF kwa mpango wake wa kuwafikia wakulima na wachimbaji wa madini ambapo hadi sasa
wakulima 29,000 wachimbaji madini 7000 wamejiunga na NSSF na wanafaidika na mafao yanayotolewa.
Uzoefu wa
NSSF unatuonyesha kwamba wananchi wengi wamekosa tu uelewa na taarifa sahihi. Wakumbusheni
kuwa hifadhi ya jamii si jambo jipya au la kigeni, hata katika jamii
zetu kabla ya kuja kwa mifumo hii rasmi, kumekuwepo na utaratibu wa jamii
kujiwekea mifumo ya hifadhi ya jamii. Katika jamii zetu kumekuwa
na utaratibu wa kuwahudumia wazee, wasiojiweza na watoto. Mtu hakupoteza
heshima na thamani yake katika jamii kwa kuwa amepoteza uwezo wake wa kuchangia
katika jamii, ama kwa kustaafu, kwa ajali au kwa kutojaaliwa uwezo wa
kuchangia.
Mabadiliko ya kidunia yameifanya mifumo hiyo sasa
isiweze kuhimili jukumu hilo. Hivyo, mifuko ya hifadhi ya jamii ndio mbadala na
salama ya ustawi wa mtu katika dunia ya leo. Wakumbusheni kuwa shida na majanga
huwafika watu wakati ambao hawajajiandaa. Hivyo, ni vyema kujisitiri kabla
hujasitiriwa.
Ndugu wadau wa hifadhi ya jamii,
Ni vizuri kukumbushana pia kwamba, uhai wa mifuko ya hifadhi ya jamii unategemeana
pia na uendelevu wa michango ya wanachama. Hivyo, hatuna budi pia kutoa
kipaumbele katika kuelimishana juu ya umuhimu na wajibu wa waajiri kuwasilisha
michango ya wanachama kwa wakati. Mifuko ya hifadhi ya jamii inatakiwa
kuhakikisha inakusanya michango ya wanachama wake bila ajizi. Wahamasisheni
wanachama wa mifuko juu ya umuhimu wa kuhakikisha michango yao inawasilishwa,
na inabaki katika mifuko ya hifadhi ya
jamii ili iwafae wakati wa matatizo na maisha ya uzeeni. Waelemisheni juu ya
athari ya tabia ya sasa ya baadhi ya watumishi kuamua kushirikiana na waajiri
wasio waaminifu kutopeleka michango hiyo, au baadhi ya wanachama kujitoa katika
mifuko ya awali pale inapotokea amebadilisha ajira kutoka kwa mwajiri mmoja
kwenda kwa mwingine.
Mchango wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
kuelekea Dira ya 2025
Ndugu Wadau wa Hifadhi ya Jamii;
Mifuko ya hifadhi ya jamii ina wajibu
mkubwa wa kuchangia juhudi za Serikali katika kufikia dira yetu ya kuwa nchi
yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Mifuko hii imeonyesha uwezo wa kuwekeza katika sekta na miradi ya
uwekezaji wa muda mrefu ambayo sekta binafsi imekuwa ikikwepa. Miradi ya aina
hii kama miundombinu msingi na nishati ndio inayoweza kukwamua nchi katika
umasikini, na kuleta mapinduzi kimaendeleo.
Uzoefu huu unashawishi kuwa mifuko hii sasa
itazame katika sekta ya Kilimo. Kilimo ndio sekta mama ya uchumi wetu na
inaajiri zaidi ya asilimia 70 ya
wananchi wetu, lakini ukuaji wake ni asilimia
4.4 ambayo ni chini ya kiwango kinachotakiwa cha asilimia 6 kwa mwaka kutokana na kukosa uwekezaji wa kutosha. Ndio
sababu, pamoja na kasi nzuri ya ukuaji wa uchumi ya wastani wa asilimia 7, umasikini umepungua kwa asilimia 2 tu.
Umasikini huzuia pia kasi ya ukuaji wa
mifuko ya hifadhi ya jamii. Hivyo, uwekezaji wenu katika sekta itakayosaidia
kuondoa umasikini, ni kujitengenezea pia fursa kwa mifuko yenu kupata wanachama
wengi zaidi siku za usoni. Tumeshuhudia namna ambavyo uwekezaji wa pamoja wa NSSF, PPF na PSPF
wa kiasi cha asilimia 45
katika Kiwanda cha Sukari cha Kagera kumezalisha ajira 3,500. Mbali na ajira, wataalam wanasema pia kuwa katika kila
shilingi moja inayowekezwa vizuri kwenye kilimo, huzalisha faida ya hadi shilingi 3.2. Nawatia shime muangalie
uwezekano wa kuwekeza katika kilimo hususan kwenye viwanda vya pembejeo za
kilimo na vya kusindika na kuongeza
thamani ya mazao. Tukiweza kuongeza
thamani na kuepuka kuuza nje mazao ghafi, tutakuwa tumewatoa Watanzania wengi
kutoka kwenye umasikini na mifuko yetu itapata wanachama wengi zaidi na wenye
uwezo mkubwa zaidi wa kuchangia mifuko hiyo.
Hitimisho
Ndugu wadau wa hifadhi ya jamii,
Kwa kumalizia napenda kwa mara nyingine
tena kukushukuru Mheshimiwa Waziri kunialika na nikupongeze kwa namna unavyilea
vizuri mifuko yetu ya hifadhi ya jamii. Nakupongeza Mwenyekiti wa Bodi ya NSSF
kwa uongozi wenu mzuri. Natoa pongezi
nyingi kwa Mkurugenzi Mkuu, Dkt.
Ramadhani Dau kwa kazi nzuri unayoifanya, na mafanikio makubwa yaliyopatikana
katika NSSF chini ya uongozi wako. Nifikishie pongezi hizi pia menejimenti na
wafanyakazi wote wa NSSF. Kazi mnayoifanya inaonekana na tuna matarajio ya
kuona mengi na makubwa zaidi miaka hamsini ijayo.
Baada ya kusema hayo, napenda kutangaza
kwamba mkutano huu wa nne wa wadau wa Shirika la Taifa Hifadhi ya Jamii (NSSF)
umefunguliwa rasmi. Nawatakia mkutano mwema.
Ahsanteni sana kwa
kunisikiliza.
MHESHIMIWA Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia;
Mheshimiwa Balozi Mwanaidi Maajar, Mwenyekiti wa
Bodi ya
Wakarugenzi wa Kampuni ya Vodacom Tanzania;
Ndugu Ndewirwa Kitomari, Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi
ya Benki ya CBA;
Waheshimiwa Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa;
Ndugu Isaac Mwuondo – Mkurugenzi Mtendaji CBA;
Ndugu Rene Meza, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nakushukuru sana Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa,
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na viongozi wa Vodacom na CBA kwa
kunialika kuja kujumuika nanyi kwenye sherehe hii adhimu ya kuzindua huduma
mpya ya fedha kwa njia ya simu nchini ijulikanayo kama M-Pawa. Huduma ambayo
itazidi
kurahisisha na kurasimisha malipo ya fedha,
kuchochea utamaduni wa kuweka akiba, na
kupanua wigo wa wananchi kufikiwa na huduma ya fedha.
Nawapongeza Vodacom na CBA kwa kutudhihirishia jinsi ambavyo huduma za benki na huduma za simu za mkononi zinavyoweza kutegemeana, kuunganishwa na kufanya kazi kwa pamoja. Kwa kufanya hivyo mnaweza kuwafikia Watanzania wengi na kuwapatia huduma za kifedha kwa njia rahisi na nafuu kupitia simu za mkononi. Aidha, wateja wenu watakuwa na akaunti zao benki na kuweza kuzitumia kwa kutumia simu zao za mkononi. Hongereni sana.
Mabibi na Mabwana;
Huduma hii ya M-Pawa ni nyenzo muhimu inayowezesha dhamira ya Serikali ya kutaka Watanzania wengi wafikiwe na kujumuishwa katika huduma rasmi za kifedha (financial inclusion). Lengo la Serikali ni kuona kuwa asilimia 50 ya watu wazima nchini wanatumia huduma za kibenki ifikapo mwaka 2016. Haya ndiyo matakwa ya Tamko la Maya, Mexico mwaka 2011, kuhusu kuwawezesha wananchi kuingia katika mfumo rasmi wa kifedha (Alliance for Financial Inclusion Global Initiative). Kwa ubunifu wa namna hii naamini lengo hilo tutalifikia.
Mabibi na Mabwana;
Taarifa zinaonesha kuwa hadi kufikia mwaka 2012, ni
asilimia 17 tu ya Watanzania, ambayo
ni sawa na watu wazima milioni 3.7 tu
ndiyo waliokuwa na akaunti za benki. Kwa
mujibu wa utafiti wa Benki ya Dunia (Global Findex 2012), wakati huo Tanzania
ilikuwa nyuma ya wastani wa Afrika ambao ulikuwa asilimia 24. Pia tulikuwa nyuma ya Uganda ambayo ilikuwa imefikia asilimia 20 na Kenya ambayo ilikuwa asilimia 42. Kuanza kwa matumizi ya
teknolojia ya kutoa huduma ya fedha kwa njia ya simu ya mkononi imekuwa kichocheo
kikubwa cha mabadiliko. Kumewezesha Watanzania milioni 9.8 ambayo ni sawa na asilimia 43 kuingia kwenye mfumo rasmi wa fedha kwa kuwa na akaunti za fedha
kwenye simu ilipofika mwaka 2013. Utafiti wa karibu wa FinScope Tanzania na FinScope
Kenya idadi ya sasa ni watu milioni 12 ambayo ni sawa na asilimia 57 ya Watanzania watu wazima kuingia kwenye mfumo rasmi wa
fedha kwa kuwa na akaunti za benki au za simu. Haya ni mafanikio makubwa na ya
kujivunia. Tutalifikia lengo la asilimia
50 ifikapo 2016.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa bado fursa ni pana sana ya kuwezesha Watanzania wengi zaidi kunufaika na mifumo rasmi ya fedha kwani hivi sasa Watanzania milioni 30 wanatumia simu za mkononi. Utafiti uliofanywa na Wizara ya Viwanda na Biashara wakati wa mapitio ya Sera ya Biashara Ndogo na Kati (SMEs) iliyofanyika mwaka 2013 inaonesha kuwa, kati ya SMEs milioni 3 zinazokadiriwa kuwepo nchini, ni SMEs 620,000 tu, yaani asilimia 20 ndizo zinazotumia mfumo rasmi wa fedha. Asilimia 12 ya SME’s zinatumia mifumo ya kijamii/kienyeji na asilimia 70 hazitumii kabisa mifumo ya fedha. Hii inaonesha kuwa kuna fursa kubwa bado ya kuingiza asilimia 80 waliobakia kwenye huduma rasmi ya fedha. Natoa wito kwa mabenki na taasisi nyingine za fedha pamoja na makampuni ya simu kuongeza kasi ya kuwahamasisha Watanzania kujiunga na mifumo rasmi ya fedha.
Mheshimiwa Waziri;
Mabibi na Mabwana;
Nawapongeza Vodacom na Benki ya CBA kwa ubunifu wao uliozaa huduma ya M-Pawa tunayoizindua leo. Huduma hii inaboresha zaidi huduma tuliyoizoea ya M-Pesa kwa kuwa sasa inaileta benki mkononi mwa mteja. Inamuwezesha mtu kuweka akiba, kufanya malipo na kwa mara ya kwanza kukopa fedha kwa kutumia simu yake ya mkononi.
Ni matumaini yangu kuwa M-Pawa na mifumo mingine ya teknolojia ya habari inayofanana nayo itawahamasisha wananchi kuondokana na utamaduni wa kutunza fedha mchagoni na kuziweka katika njia salama zaidi. Kwa njia hii, tutaweza kujenga utamaduni wa kuweka akiba ya fedha ambao baadaye unaweza kuwa chachu katika ukuzaji uwekezaji hapa nchini.
Mabibi na Mabwana;
Huduma ya M-Pawa inajiunga na huduma zingine za fedha zilizopo ambazo tayari zimewanufaisha wananchi wengi. Watanzania zaidi ya milioni 10 sasa wanatumia huduma za fedha kupitia simu ya mkononi, na wanafanya miamala ya wastani wa shilingi trilioni 2 kwa mwezi.
Mabibi na Mabwana;
Ili mpango huu ufanikiwe kusambaa nchini kote tunahitaji kuwa na mifumo rasmi ya utambuzi, uhakiki na uthibiti wa wateja na taarifa muhimu zinazowahusu. Serikali itaendelea kufanya kazi na wadau wote wanaohusika katika sekta ya fedha pamoja na vyombo vya usalama na udhibiti kuhakikisha kwamba watu wetu wanakuwa na namna bora ya kutambulika. Hii itawaondolea ninyi watoa huduma hatari ya kuibiwa fedha na wateja wasio waaminifu. Ni matumaini yangu kuwa mifumo hiyo itakamilika mapema iwezekanavyo. Natambua kwamba kukamilika kwa zoezi la kuwapatia Watanzania vitambulisho kutasaidia sana kufanikisha mifumo ya utambuzi. Napenda kutumia nafasi hii kuwakumbusha ndugu zetu wanaotoa vitambulisho vya taifa kuongeza kasi ya utoaji wa vitambulisho kwa Watanzania.
No comments:
Post a Comment