Na Mwandishi Maalumu
SERIKALI imetoa ufafanuzi
kuhusu taarifa potofu zinazoendelea kuchapishwa na kutangazwa kwenye baadhi ya
vyombo vya habari kuhusu Watumishi Waandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii,
Prof. Alexander Songorwa ambaye ni Mkurugenzi, Idara ya Wanyamapori na Prof.
Jafari Kideghesho, Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Matumizi Endelevu ya
Wanyamapori.
Kumekuwa
na taarifa kwenye baadhi ya vyombo vya habari kwamba Wakurugenzi hao walikuwa
wamefukuzwa kazi na Waziri wa Maliasili na Utalii, na kisha kurejeshwa kwa
maelekezo ya Ikulu. Taarifa hizo si sahihi.
Ukweli
ni kwamba Prof. Alexander Songorwa na Prof. Jafari Kideghesho hawajawahi
kufukuzwa kazi ama kuadhibiwa. Hatua za kinidhamu katika Utumishi wa Umma zina taratibu na miongozo yake, inayotawaliwa na
nyaraka kuu nne, miongoni mwa nyingine, kama ifuatavyo:
·
Sera ya Menejimenti na Ajira katika
Utumishi wa Umma ya Mwaka 1999;
·
Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya Mwaka
2002 (kama ilivyorekebishwa mwaka 2008);
·
Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003;
·
Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma
za Mwaka 2009.
Kwa mujibu wa
nyaraka hizo, na kwa mujibu wa sheria, kila mtumishi wa umma anayo mamlaka yake
ya ajira na mamlaka yake ya nidhamu.
Mamlaka ya nidhamu
ya Prof. Alexander Songorwa na Prof. Jafari Kideghesho haijawahi kuwachukulia hatua zozote za kinidhamu. Lakini,
baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii kuonyesha kutoridhika na utendaji wao,
Mamlaka yao ya nidhamu iliwaruhusu kuchukua likizo zao za mwaka za kawaida.
Likizo zao zilipoisha walirejea kazini kama kawaida.
Hata hivyo,
kutokana na yaliyokwisha kutokea, wanataaluma hawa, Prof. Alexander Songorwa na
Prof. Jafari Kideghesho, kwa hiari yao wenyewe, wamekubali kuchukua majukumu
mengine katika Utumishi wa Umma kama watakavyopangiwa.
No comments:
Post a Comment