Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete amesema
kuwa kuwekeza katika chanjo ni moja ya uwekezaji wa maana zaidi na wa akili
zaidi ambao mataifa yanaweza kufanya katika kuboresha afya ya raia wake na hali
ya baadaye ya mataifa duniani.
Aidha,
Rais Kikwete amesema kuwa afya bora ni msingi mkuu wa ujenzi wa jamii zenye
chumi bora na kuwa afya ni maendeleo.
Rais
Kikwete ameyasema hayo Alhamisi, Mei 8, 2014 wakati aliposhiriki katika
Uzinduzi wa Azimio la Viongozi wa Afrika wa Mpango wa Chanjo za Watoto wa
Afrika hadi Mwaka 2020 Unaosimamiwa na Mpango wa Pamoja wa Dunia wa Chanjo
(GAVI - Alliance) kwenye Hoteli ya Transcorp Hilton mjini Abuja, Nigeria.
Azimio
hilo la Mpango huo wa Immunise Africa 2020 limezinduliwa
katika mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na Rais wa Benki ya Maendeleo
ya Afrika (AfDB) Mheshimiwa Donald Kaberuka.
Chini
ya Mpango huo, nchi za Afrika zinapanga kutumia kiasi cha dola za Marekani
milioni 700 kati ya mwaka 2016 na 2020 kwa ajili ya kugharimia chanjo zitakazonunuliwa
na GAVI. Hii ni mbali na mabilioni ya fedha ambayo nchi za Afrika zitatumia
kwenye maeneo mengine ya afya.
Kwenye
tukio hilo, Mheshimiwa Kaberuka ameungwa mkono na Rais Kikwete, Rais Macky Sall
wa Senegal na Rais John Mahama wa Ghana ambaye amewakilishwa na waziri wake wa
afya.
Rais
Kikwete amesema kwenye tukio hilo: “Azimio tunalolitoa leo ni kauli ya
kuonyesha misimamo thabiti ya viongozi wa Afrika kuwekeza zaidi katika shughuli
hii takatifu. Tunafanya hivyo kwa sababu tunatambua kuwa faida za chanjo ni
kubwa zaidi kuliko kuwa faida za kiafya.”
Ameongeza
Rais Kikwete: “ Jamii zenye afya bora zinazaa chumi zenye afya bora. Afya ni
maendeleo. Chanjo ni moja ya uwekezaji maana zaidi na wa akili zaidi ambayo
mataifa yanaweza kufanya kwa kuboresha afya ya raia wake na hali ya baadaye ya
mataifa yetu duniani.”
Dkt.
Kaberuka akizungumza kwenye tukio hilo amesema: “Nchi zinazowekeza katika
upatikanaji wa chanjo leo, watavuna matunda makubwa ya uwekezaji huo katika
muda mfupi na wa kati ujao.”
GAVI
Alliance ambayo ilianzishwa mwaka 2000 na ambayo Mwenyekiti wake wa kwanza wa
Bodi ya Wakurugenzi alikuwa Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Hayati Nelson
Mandela imesaidia kuwawezesha watoto milioni 440 kupata chanjo na kuokolewa
katika hatari ya vifo.
Faida
za GAVI Alliance zimekuwa wazi kabisa kwa Tanzania kiasi cha kwamba Septemba
mwaka jana, 2013, Taasisi ya Bill na Melinda, moja ya taasisi zinachangia fedha
nyingi katika kudumisha Mpango huo wa GAVI ilitangaza kuwa Tanzania ilikuwa
imefikia lengo la Millenia kuhusu watoto na chanjo la kupunguza vifo vya watoto
kwa theluthi mbili.
Mpaka
sasa Tanzania imefanikiwa kuchanja asilimia 93 ya watoto wake wote na miaka
miwili iliyopita, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa GAVI ambako
chanjo mbili mpya zilianza kutumika nchini ikiwa nchi ya kwanza duniani kutumia
chanjo hizo. Chanjo hizo ni ile ya homa ya mapafu na ugonjwa wa kuharisha.
Baadhi
ya nchi duniani zinazochangia katika kugharimia GAVI Alliance ni pamoja na Australia, Canada, Denmark, Ufaransa, Ujerumani,
India, Ireland, Italia, Japan, Luxembourg, Uholanzi, Norway, Russia, Jamhuri ya
Korea, Afrika Kusini, Hispania, Sweden, Uingereza na Marekani.
Taasisi
nyingine zinazogharimia GAVI Alliance ni Umoja wa Ulaya, Mfuko wa OPEC, Bill
and Melinda Gates Foundation, Lion Club International Foundation, Vodafone,
Comic Relief, Anglo American, JP Morgan na taasisi nyingine nyingi.
Wakati
huo huo, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la
Algeria, Mheshimiwa Mohamed Larbi Ould Khelifa, Mwakilishi wa Biashara wa
Marekani Mheshimiwa Michael Froman na Mwakilishi wa Kampuni ya Marekani ya General
Electric katika Afrika Bw. John Rice.
No comments:
Post a Comment