Mheshimiwa Waziri Mkuu;
Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais,
Zanzibar;
Mheshimiwa Spika wa Baraza la
Wawakilishi;
Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mawaziri
Waliopo;
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Waheshimiwa Mabalozi;
Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi;
Katibu Mkuu Kiongozi na Makatibu
Wakuu;
Viongozi wa Serikali wa Ngazi
Mbalimbali;
Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi;
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu;
Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar;
Viongozi wa Vyama vya Siasa;
Viongozi wa Madhehebu ya Dini;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Shukrani na Pongezi
Ndugu Wananchi;
Awali ya yote, naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa
kutujalia uzima
na kutuwezesha kukutana
hapa siku ya leo. Napenda pia
kuwashukuru waandaaji wa hafla hii kwa kunipa heshima kubwa ya kuzindua Chapisho la Tatu la Taarifa za Msingi za Kidemografia,
Kijamii na Kiuchumi Linalotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012.
Nakushukuru sana Mheshimiwa
Waziri Mkuu kwa maelezo yako mazuri ya awali kuhusu Chapisho hili. Nakupongeza
wewe, pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa uongozi wenu mzuri wa
zoezi la Sensa. Chapisho tunalozindua leo ni matunda ya kazi nzuri mliyoifanya
ya kuziongoza Idara za Takwimu za Serikali zetu mbili ambazo ndizo
zilizosimamia na kuendesha zoezi lenyewe la sense ya watu na makazi.
Sensa inaendeshwa kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha Sheria ya Takwimu
(the Statistic Act) sura ya 351. Katika kipindi chote cha miaka 50 ya Muungano wetu tumefanya Sensa mara
tano, mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.
Umuhimu wa Chapisho la
Tatu
Ndugu Wananchi;
Sensa ni zoezi pana
sana. Sensa ni zaidi ya kuhesabu
watu. Sensa hujumuisha pia kukusanya na
kufanya uchambuzi wa taarifa kuhusu masuala mbalimbali ya kiuchumi na
kijamii. Taarifa hizo husaidia Serikali
katika utungaji wa sera na kutengeneza mipango na mikakati ya maendeleo nchini. Tangu kufanyika kwa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, Idara Kuu ya Takwimu ya Taifa na Idara ya
Takwimu Zanzibar ambazo
ndizo zilizohusika na zoezi hili zimeendelea kutoa matokeo
kulingana na kalenda ya utoaji wa matokeo ya Sensa. Matokeo ya mwanzo nilitolewa tarehe 31 Desemba, mwaka 2012 kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja. Siku ile nilitangaza jumla
ya idadi ya watu nchini Tanzania. Chapisho la pili lilihusu mgawanyo wa watu
kwa umri na jinsi ambalo lilitolewa tarehe 25 Septemba, 2013.
Chapisho la Tatu ninalolizindua
leo linatoa taarifa za msingi za kidemografia (mnyumbuliko wa idadi ya watu),
kijamii na kiuchumi zinazotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Taarifa za Chapisho la Tatu zina umuhimu wa
aina yake. Zinaonesha Tanzania imepiga hatua kiasi gani katika
maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Aidha, upatikanaji
wa taarifa katika kipindi hiki utaviwezesha vizazi vijavyo kuifahamu Tanzania ilivyokuwa mwaka 2012.
Muhtasari wa Matokeo ya
Chapisho la Tatu
Ndugu Wananchi;
Sensa ya Mwaka 2012
imefanyika katikati ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Miaka 5 (2011-2016).
Mpango huu tunaoendelea kuutekeleza una lengo la kutufikisha kwenye Dira ya
Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 na ile ya Zanzibar ya mwaka 2020 ambapo
tunatarajia kuwa nchi yetu itakuwa imefikia uchumi wa kati. Kwa utaratibu huu
wa kufanya Sensa kila baada ya miaka 10, ina maana kuwa Sensa inayofuata
itafanyika mwaka 2022 ikiwa ni miaka michache kabla ya kufikia Dira ya Taifa.
Hivyo, matokeo haya ni msingi wa kupima mwelekeo wetu kiuchumi na kijamii
kufikia lengo letu la kuwa uchumi wa kati ifikapo 2020 kwa upande wa Zanzibar
na 2025 nchi nzima.
Chapisho hili lina takwimu
nyingi sana kuhusu nyanja mbalimbali za maisha ya Watanzania. Takwimu hizi
zinatupa fursa ya kujua maeneo tunayofanya vizuri na yale tunayohitajika
kuyaimarisha. Vilevile, zinatuonyesha yale maeneo ambayo tulidhani tunafanya
vizuri lakini kumbe siyo, hivyo basi tunatakiwa kuyawekea mkakati maalum. Hali
kadhalika, taarifa zinatuamsha kuona yale
maeneo mapya ambayo hatukuwahi kuyafikiria lakini sasa tunapaswa
kuyaangalia kwa karibu.
Kwa ujumla, kulingana na
takwimu za Sensa ya 2012, idadi ya watu Tanzania iliongezeka kutoka watu milioni 34.4 mwaka 2002 hadi watu milioni 44.9 mwaka 2012. Hii ni sawa na kasi ya ongezeko la asilimia 2.7 kwa mwaka. Kwa kasi hii ya ongezeko la watu, Tanzania Bara inatarajiwa kuwa na watu milioni 63.3 mwaka
2025 ambao ndiyo mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Dira ya
Maendeleo 2025 kwa Tanzania Bara. Aidha, Zanzibar inatarajiwa kuwa na watu milioni 1.8 ifikapo mwaka 2020 ambao ndiyo mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo
ya Zanzibar. Kwa kasi hii ya ongezeko la idadi ya watu Tanzania inatarajiwa kuwa na watu milioni
125 mwaka 2050.
Ndugu Wananchi;
Ili kufikia dira zetu za
maendeleo, yaani ya mwaka 2020 kwa Zanzibar na ya mwaka 2025 kwa nchi nzima
ambapo tutakuwa na idadi ya watu takribani
milioni 65.1, inatupasa kujitazama tulipotoka na tulipo leo. Kwa mujibu wa
Chapisho hili la Tatu, tumepiga hatua kubwa na nzuri katika maeneo mengi, na
hivyo kuashiria kuwa tuko katika mstari sahihi kuelekea Tanzania tunayoitamani.
Baadhi ya takwimu hizi kwa ufupi ni zifuatazo:
i.
Zaidi ya asilimia 90 ya watu wote Tanzania
walizaliwa baada ya Muungano wa mwaka 1964. Tafsiri yake ni kwamba idadi kubwa
ya Watanzania ni vijana ambao wamezaliwa, kukua na kufaidika na matunda ya
Muungano. Hiki ni kiashiria kikubwa kuwa tumeweza
kujenga utaifa mpya, yaani utanzania katika miaka 50 ya Muungano wetu.
ii.
Hii ni Sensa ya tano tangu Muungano wetu mwaka 1964. Sensa ya kwanza ilikuwa mwaka 1967, ya pili
mwaka 1978, ya tatu mwaka 1988, ya nne mwaka 2002 na ya tano 2012. Takwimu za Sensa za kati ya mwaka 1967 na mwaka 2012 zinaonesha kuwa
idadi ya watu wa
Tanzania ambao
wanaishi mijini imeongezeka kutoka asilimia
6 mwaka 1967 hadi asilimia 30 mwaka 2012. Ukuaji huu wa miji ni kiashiria muhimu kuwa
safari yetu ya kuelekea uchumi wa katini ya uhakika. Hatuna budi sasa, sera na mikakati yetu
kuielekeza katika kuhakikisha miji yetu inao uwezo wa kuhimili ongezeko hili la
watu kwa maana ya utoaji wa huduma za kijamii na ajira.
iii.
Katika
kipindi cha miaka 50 wastani wa umri wa kuishi kwa mtoto wa Kitanzania
anayezaliwa umeongezeka kutoka miaka 41 mwaka 1967 hadi kufikia miaka 61 mwaka
2012. Maana yake ni kuwa, huduma za afya
zimeimarika, watu sasa wanaishi kwa muda mrefu zaidi kuliko ilivyokuwa
awali. Hata hivyo, bado hatujafikia
viwango vya wenzetu wa Asia na Ulaya ambao wastani wao ni miaka 70 na
kuendelea.
iv.
Vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka vifo 115 kati ya kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai mwaka 1988 hadi kufikia vifo 45 mwaka 2012. Na, mwaka 2013 tumefikia
21. Vifo vya watoto chini ya miaka 5
vimepungua kutoka 231 mwaka 1988
hadi 68 mwaka 2012 na 2013 tumefikia
vifo 54 kwa 1,000. Pia, idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi imepungua
kutoka vifo 578
kwa kila akina mama 100,000 wanaojifungua
mwaka 2004/2005 hadi 454 mwaka 2010 na kwa mujibu wa takwimu za Sensa,
vifo hivi vimeendelea kupungua hadi 432
mwaka 2012. Hii ni hatua kubwa kuelekea lengo la Milenia ya Mwaka 2015 ya vifo
193.
v.
Asilimia ya
kaya zinazopata maji safi ya kunywa imefikia asilimia 57 mwaka 2012. Vile
vile, kaya zinazotumia umeme kama nishati ya kuangazia zimeongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2002 hadi asilimia
21 mwaka 2012.
vi.
Kwa upande wa sekta ya elimu, asilimia ya watu wenye umri wa miaka 10
na zaidi wanaojua kusoma na kuandika kwa Tanzania Bara imeongezeka kutoka asilimia 31 mwaka 1967 hadi kufikia asilimia 78 mwaka 2012. Kwa Zanzibar
kiwango hiki kimeongezeka kutoka asilimia
39 mwaka 1967 hadi asilimia 86
mwaka 2012.
vii.
Takwimu
zinazoonesha kwamba umaskini wa kipato umepungua kutoka asilimia 33.6 mwaka 2007 hadi asilimia
28.2 mwaka 2012.
viii.
Takwimu zinaonesha kwamba makazi ya wananchi wote wa Tanzania
yaliyojengwa kwa vifaa vya kisasa (zege, mawe, saruji na vyuma) yameongezeka. Familia zinazoishi kwenye nyumba za bati
zimeongezeka kutoka asilimia 46
mwaka 2002 hadi asilimia 65 mwaka
2012.
ix.
Vilevile, umiliki wa simu za kiganjani umeongezeka sana. Mwaka 2012 wastani ulikuwa ni asilimia 64
ikilinganishwa na asilimia 10 mwaka 2005. Kuongezeka kwa simu ni kiashiria cha
kuongezeka kwa biashara, idadi ya watu wanaotumia huduma za kifedha kwa njia ya
simu na urahisi wa mawasiliano ambao unawezesha usambazaji wa taarifa za
kijamii na kibiashara katika maeneo mengi hivi sasa.
Mazingatio Yatokanayo na Chapisho la Tatu la Sensa
Ndugu Wananchi;
Ufupi au urefu wa safari
unaweza kuujua tu iwapo unafahamu unapotoka, ulipo na unapokwenda. Taarifa ambazo zimewasilishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonesha
kuwa tumepata mafanikio ya kuridhisha katika maeneo mengi, na kuwa tumekuwa
tunasonga mbele mwaka hadi mwaka na siyo kurudi nyuma. Kwa hiyo
matokeo haya yanapaswa kuwaongoza Viongozi na Watendaji wa ngazi zote katika Serikali Kuu na Serikali za
Mitaa kujua maeneo ambayo kasi ya utekelezaji wa programu za maendeleo kwa wananchi ilikuwa ndogo, na hivyo kustahili kupewa msukumo mpya katika utekelezaji wake.
Ndugu Wananchi;
Nimefarijika kusikia kuwa taarifa za Sensa
zinaonesha hatua
kubwa tuliyopiga katika kuleta usawa wa kijinsia kati ya wanaume na wanawake. Ingawa viashiria vingi bado vinaonekana bora zaidi kwa wanaume kuliko wanawake, lakini pengo kati yao limepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma. Kwa mfano, asilimia ya wanaume wenye umri
wa miaka 10 na zaidi wanaojua kusoma na kuandika ilikuwa asilimia 45 kwa Tanzania Bara na asilimia 55
kwa Zanzibar mwaka 1967. Kwa upande wa
wanawake ilikuwa asilimia 19 na asilimia 23 kwa Tanzania Bara na Zanzibar mwaka 1967. Taarifa
za Sensa ya Mwaka 2012 zinaonesha kuwa pengo hili limepungua sana. Wanaume wenye umri wa miaka 10 na zaidi wanaojua
kusoma na kuandika kwa mwaka 2012 ni asilimia
82 ya wanaume wote kwa Bara ukilinganisha na asilimia 75 kwa wanawake. Kwa upande wa Zanzibar, idadi ya wanaume
wanaojua kusoma na kuandika ni asilimia
89 ya wanaume wote kulinganisha na asilimia
83 ya wanawake.
Hatuwezi kupata maendeleo
makubwa na endelevu bila kuhakikisha usawa wa kijinsia. Wanawake ni asilimia 51 ya Watanzania wote, hivyo, hatuna namna yoyote tunayoweza
kulipuuza kundi hili kubwa, ambalo ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu wote
katika shughuli za maendeleo. Ndiyo
maana, tumeelekeza juhudi kubwa kurekebisha kasoro hii ya kihistoria na kimfumo
kwa kuwapa wanawake fursa ili nao washiriki sawia katika shughuli za maendeleo
katika ngazi ya familia, jamii na hata taifa.
Ni vyema ikaeleweka kuwa hatuwapendelei wanawake bali tunawapatia kile
wanachostahili kupata kama raia na kama wanadamu. Stahili ambazo wamekuwa wakizikosa kwa miaka
mingi.
Serikali itaendelea kuimarisha juhudi za
utekelezaji wa Sera ambazo zinalenga kuhakikisha kuwa pengo hili linazibika ili
Watanzania wote wafaidike na rasilimali za Taifa bila
ya kujali jinsia zao.
Maelekezo kwa Tume ya Taifa ya Takwimu
Ndugu Wananchi;
Nimesema hapo awali kuwa lengo kubwa la kufanya
Sensa ni kutoa takwimu ambazo zitachangia katika jitihada za kuboresha maisha
ya Watanzania. Taarifa za sensa ambazo
zitasaidia kuboresha sera za nchi kwa mambo mbalimbali, kupanga na kutathmini
programu za maendeleo na uimarishaji wa utoaji wa huduma za jamii. Lengo hili haliwezi kufikiwa ikiwa taarifa za
sensa na nyinginezo kwa ujumla wake hazitawafikia watumiaji wote wanaozihitaji.
Ofisi za Takwimu zina jukumu la kutoa takwimu katika mfumo mzuri na lugha
rahisi na kuzisambaza na kuhamasisha matumizi yake.
Pamoja na
usambazaji wa taarifa za sensa kwa vitabu na machapisho, tumieni tovuti na njia
nyingine za kisasa kusambaza taarifa zenu. Ninafarijika kusikia kwamba tayari
mmeanza juhudi hizi, kwani uzinduzi wa Chapisho hili la tatu utaenda sambamba
na uzinduzi wa usambazaji wa taarifa kwa njia ya mtandao.
Ofisi za Takwimu zimetimiza wajibu wake wa kutoa
takwimu na sasa ni jukumu la Wizara, Idara,Taasisi za Serikali na watumiaji
wengine wote kuzifanyia kazi. Natoa agizo kwa viongozi ngazi zote za utawala
kutafsiri matokeo haya kwa kuoanisha na utekelezaji wa sera na programu za
maendeleo ya kisekta katika maeneo yao. Matokeo haya ya Sensa sasa ndiyo rejea
yetu ya takwimu katika mipango yetu ya utekelezaji. Kile kisingizio cha kukosekana kwa takwimu
mpya sasa kimefikia ukomo. Takwimu ni
kitendea kazi, sasa mnazo na mkazifanyie kazi, siyo kuendeleza semina za
kujadili matatizo na mapungufu. Takwimu
zimetuonyesha mafanikio tuliyoyapata na mapungufu yaliyopo ambayo mkayatatue na
siyo kuyajadili.
Wito kwa Wananchi na Wadau
Ndugu Wananchi;
Napenda pia kutoa wito kwa
wananchi na wadau wa maendeleo hasa asasi za kiraia kusoma taarifa hizi na
kuzitumia vizuri. Kumekuwepo na
upotoshaji mkubwa sana wenye kubeza mafanikio yaliyopatikana nchini kutokana na
jitihada za Serikali na wananchi kwenye kuleta maendeleo. Taarifa hii inaweka wazi ukweli ulivyo. Zitumieni.
Kama upotoshaji ulikuwa ni kwa sababu ya kukosekana kwa rejea ya takwimu
sahihi, takwimu ndizo hizo kwa kila mmoja wetu kuziona na kuzitumia. Asiyefanya hivyo ana lake jambo.
Hitimisho
Ndugu Viongozi Wenzangu;
Ndugu Wananchi;
Niruhusuni nirudie tena
kuwashukuru washirika wetu wa maendeleo waliotusaidia kufanikisha zoezi la
Sensa ya watu na makazi. Kwa namna ya
pekee nawashukuru Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Shirika la Maendeleo la
Uingereza (DFID), Taasisi za Umoja wa Mataifa ikiwemo UNFPA, UNDP na
UNICEF. Nawashukuru tena Mheshimiwa
Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda na Makamu wa Rais wa Zanzibar, Balozi Ali
Seif Idd kwa uongozi wenu mzuri uliowezesha zoezi zima la sensa
kufanikiwa. Pia, nawapongeza viongozi na
watendaji wa Idara zetu mbili za Takwimu kwa kazi kubwa na nzuri
waliyofanya. Umakini na umahiri wao
ndiyo uliotufikisha hapa. Nawashukuru na
kuwapongeza viongozi wote wa Serikali wa ngazi zote za utawala ambao walishiriki
kwa ukamilifu katika maandalizi na hatimaye utekelezaji wa Sensa ya Mwaka 2012.
Nitoe pia shukrani kwa viongozi wa vyama vya siasa, madhehebu ya dini na
mashirika yasiyo ya Kiserikali kwa ushiriki wenu hasa kwenye hatua ya
uhamasishaji wa ushiriki wa umma. Nawashukuru wadau wetu wa maendeleo kwa
michango yao muhimu ambayo imesaidia kufanikisha sensa hii.
Shukrani za kipekee ziwaendee Wananchi wote
ambao walijitokeza kuhesabiwa na kujibu maswali ya sensa kwa ufahamu mkubwa.
Kukubali kwao kushiriki ndiko chanzo kilichowezesha kupatikana taarifa tunazozindua
leo na nyingine zitakazofuata. Ni dhahiri kuwa Serikali yetu imetimiza kwa
ufanisi jukumu la kufanya Sensa ya Watu na Makazi nchini. Lengo limetimia la kujua hali halisi ya
rasilimali watu iliyopo Nchini kama zilivyofanya Awamu zote zilizotangulia.
Ndugu Wananchi;
Baada ya kusema maneno haya
ya utangulizi, sasa, kwa heshima na taadhima kubwa, napenda kutamka kwamba Chapisho
la Taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi linalotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 Pamoja na Matumizi ya Tovuti katika kupata taarifa
mbalimbali za Sensa ya Watu na Makazi limezinduliwa rasmi.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa kunisikiliza!
No comments:
Post a Comment