Na Mwandishi Maalumu
RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete asubuhi ya
leo, Alhamisi, Julai 3, 2014, amemkaribisha Ikulu, Dar Es Salaam, Mwana wa
Mfalme wa Japan, Prince Akishino pamoja na mkewe Princess Akishono.
Mwana
Mfamle huyo ambaye anatembelea Tanzania, amewasili Ikulu kiasi cha saa nne
asubuhi na kufanya mazungumzo ya zaidi ya nusu saa na Mheshimiwa Rais Kikwete.
Katika
mazungumzo yao, Rais Kikwete amesema kuwa Japan ni mshirika mkubwa na muhimu
sana wa maendeleo ya Tanzania. “Tunathamini sana mchango wenu katika
maendeleo ya Tanzania na tunaendelea kuwashukuru sana. Ukizunguka nchini mwetu
utaona kwa macho yako miradi mingi na mikubwa ambayo imejengwa ama inajengwa kwa
msaada wa Japan.”
Rais
kikwete ameongeza: “Pamoja na ushirikiano huu. Bado tunaamini kuwa Japan inaweza kusaidia
zaidi Tanzania hasa kwa kushawishi makampuni yake kuwekeza katika sekta
binafsi. Ukipita mitaa ya Dar es Salaam, magari tisa kati ya 10 ni ya Kijapan.
Ukiingia katika maduka ya vyombo vya elektroniki - televisheni, kompyuta, camera, karibu kila
kitu kinatoka Japan. Hali hii inathibitisha kuwa bidhaa vya Japan zina soko
kubwa na zinaweza kuzalishwa hata hapa nchini na makampuni binafsi.”
Rais
Kikwete pia ameitaka Japan kuangalia jinsi gani inavyoweza kusaidia ongezeko la
watalii kutoka Japan kuja kutembelea Tanzania kwa kuanzisha safari za ndege za
moja kwa moja kutoka huko hadi Tanzania na nchi nyingine za Afrika.
“Wataalii
wengi kutoka Japan wanashindwa kuja Afrika kwa sababu hakuna shirika hata moja
la ndege la Japan ambalo lina safari za kuja Afrika, hata Afrika Kusini hakuna.
Hii ndiyo maana hatuoni watalii wengine kutoka nchi za kusini mashariki mwa
Bara la Asia kutembelea vivutio vyetu vya utalii,”
amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kama
kuna jambo halionekani sasa katika uhusiano wa Tanzania na Japan ni uwekezaji
katika sekta binafsi. Hili ndilo jambo tunaloliomba.”
No comments:
Post a Comment