Na Mwandishi Maalumu
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amevipongeza vyama vinne vikuu vya siasa nchini ambavyo vimeanzisha majadiliano
ya kutafuta namna wajumbe waliosusia Bunge Maalum la Katiba wanavyoweza kurejea
Bungeni.
Aidha,
Rais Kikwete amewataka Watanzania kujiepusha na kishawishi cha kuingilia
mchakato wa Katiba Mpya kwa maneno na kutoa kauli nyingi, nyingine zikiwa za
upotoshaji na uchochezi, jambo ambalo linawanyima utulivu wajumbe wa Bunge
Maalum la Katiba.
Rais
Kikwete pia amewataka viongozi wa dini kuwaombea wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba
waliosusia mchakato wa kutafuta Katiba kurudi Bungeni ili kumaliza kazi ya
Kutunga Katiba Mpya kama wanavyotarajiwa na Watanzania.
Ili
kuhakikisha kuwa kazi hiyo ya Kutunga Katiba Mpya inakamilika bila wajumbe
kulazimika kufanya kazi hiyo kwa haraka kupita kiasi, Rais Kikwete ameliongezea
Bunge hilo maalum siku 60 za ziada kwa mujibu wa mamlaka ambayo anapewa na
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Rais
Kikwete ameyasema hayo leo, Jumapili, Julai 13, 2014 wakati alipohutubia mamia
kwa mamia ya waumini wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) kwenye
Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, katika maadhimisho la Kanisa hilo kutimiza miaka
75 tokea kuanzishwa nchini.
Katika
hotuba yake ambako amezungumzia masuala mbali mbali likiwemo lile la Katiba
Mpya, Rais Kikwete amewaambia wananchi waliofurika uwanjani humo:
“Bahati
nzuri wiki iliyopita, wawakilishi wa vyama vya CCM, CHADEMA,CUF na NCCR-Mageuzi
wamekuwa wanakutana kwa jitihada za Msajili wa Vyama vya Siasa. Naambiwa bado
wanaendelea na mazungumzo. Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati
kwa viongozi wa vyama hivyo kwa uamuzi wao
wa kukutana nakutafuta namna ya kusonga mbele. Tunatoa pongezi maalum
kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Mheshimiwa Jaji Mutungi kwa kufanya uamuzi
mzuri wa kuwakutanisha viongozi hao.”
Ameongeza
Rais Kikwete: “Wao ndio walitufikisha hapa na wao ndiyo wenye uwezo wa kutukwamua.
Wao wana ufuasi mkubwa miongoni mwa Wajumbe la Bunge Maalum.”
Amesema
Rais Kikwete: “Niwaombe Watanzania wenzangu
tuwape nafasi viongozi wetu wazungumze kwa utulivu. Tuache kwanza maneno maneno
yatakayowachanganya. Maana siku hizi wasemaji wamekuwa wengi na kauli zimekuwa
nyingi, nyingine zikiwa za upotoshaji na uchochezi . Miluzi mingi humchanganya
mbwa.”
Kuhusu
nafasi ya viongozi wa dini katika suala zima la baadhi ya watu kususia Bunge
Maalum la Katiba, Rais Kikwete amesema: “Ombi langu kwa nyie viongozi wa dini ni
kwamba tuwaombee ili warudi kukamilisha kazi tuliyowatuma. Tuwaombee wote
wafanye uamuzi wa pamoja. Sote tunataka warudi kukamilisha shughuli kwa sababu
mara ya mwisho lililobakia lilikuwa ni kupiga kura tu kuhusu kipengele cha
kwanza na cha sita cha Rasimu ya Katiba Mpya.”
Ameongeza:
“Tuwaombee
wawe na mazungumzo mazuri na yenye mafanikio. Wakubaliane juu ya kuendelea na
kukamilisha mchakato katika siku 60 za nyongeza kuanzia Agosti 5, mwaka huu,
2014. Tuombe kwa nguvu zetu zote ili Bwana Mungu awaongezee viongozi hao wapate
mwafaka utakaoliwezesha Taifa kupata Katiba nzuri na inayotekelezeka, katiba
yenye kuleta umoja, mshikamano na upendo, Katiba itakayodumisha amani na utulivu
nchini na kuchohcea maendeleo ya kasi zaidi.”
Akizungumzia
masikitiko ya Kanisa la TAG kuhusu kukwama kwa mchakato wa Katiba na rai ya
Kanisa hilo kuwataka wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kurejea Bungeni,
Rais Kikwete amesema:
“Masikitiko
yenu ndiyo masikitiko yangu na ndiyo masikitiko ya Watanzania wote. Rai yenu
ndiyo rai yangu na ya Watanzania wote. Nafarijika kusikia kuwa nanyi viongozi
wa dini mkizisihi pande zote kurejea Bungeni na kumaliza tofauti zao kwa mazungumzo
ndani ya Bunge.”
No comments:
Post a Comment