UMOJA MATUKIO
Wednesday, July 16, 2014
CASTLE LAGER KUWALETA MAKOCHA WA FC BARCELONA NCHINI
Meneja Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Fimbo Butallah (katikati), akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), Dar es Salaam jana, kuhusu ujio wa makocha wawili wa Kalabu ya FC Barcelona ya Hispania kwa ajili ya kutoa mafunzo ya siku 2 kwa makocha nchini. Kushoto ni Meneja wa Bia ya Castle Lager, Kabula Nshimo na Meneja Biashara wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Peter Simon.
Tuesday, July 15, 2014
RAIS JAKAYA KIKWETE AIPONGEZA UJERUMANI KWA KUNYAKUA KOMBE LA DUNIANI
TAARIFA MAALUMU
RAIS Kikwete ametoa pongezi hizo kwa
Balozi mpya wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Mheshimiwa Egon Kochanke
ambaye amewasilisha Hati zake za
Utambulisho leo asubuhi Ikulu .
“Naipongeza Ujerumani kwa kuibuka
washindi natumaini tutashirikiana vyema katika masuala ya utamaduni hasa hasa
katika kuinua kiwango cha soka nchini Tanzania na kuzisaidia klabu za
Tanzania kuanzisha shule maalum kwa ajili ya mpira wa miguu nchini.” Rais
amesema na kuishukuru Ujerumani kwa misaada mbalimbali katika sekta za Maji,
Utalii, Usafiri wa majini na maeneo mengine ya maendeleo.
Rais pia amepokea Hati za Mabalozi
Richard Stuart Man wa New Zealand na Bw.
Claude Morel wa Ushelisheli ambao wana makazi yao Pretoria, Afrika ya Kusini na
Balozi Sander Kocsis wa Hungary mwenye makazi yake Nairobi , Kenya.
Baadae leo mchana, Rais Kikwete
amekabidhi Bendera ya Taifa kwa Timu ya Michezo ya Jumuiya ya Madola,
inayotarajiwa kufanyika Glasgow kuanzia tarehe 23 Julai hadi tarehe 3 Agasti
mwaka huu.
Hafla ya kuiaga Timu hiyo imefanyika
katika Uwanja wa Taifa jijini na kuhudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe.
Bernard Membe na Naibu waziri, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
Mhe. Juma Nkamia.
Timu ya Tanzania inatarajiwa kuondoka
kesho tarehe 16 Julai,2014 kuelekea Scotland ambapo inatarajiwa kushiriki
katika Riadha, Ngumi, Mpira wa Meza, Judo, Kuogelea, Baiskeli na Kunyanyua vitu
vizito.
Rais amewaambia washiriki waende
wakijua kuwa wana deni la kutunza heshima binafsi kama wachezaji na heshima ya
Nchi na Taifa kwa ujumla.
“Siri ya mafanikio ni maandalizi
mazuri na tumewekeza sana kwenye mafunzo na maandalizi yenu na hivyo safari hii
maandalizi yalikuwa mazuri, hivyo mna deni kubwa” Rais amesema.
Monday, July 14, 2014
RAIS JAKAYA KIKWETE AVIPONGEZA VYAMA VINNE VYA SIASA KWA KUANZA MAJADILIANO YA MUAFAKA WA KATIBA MPYA
Na Mwandishi Maalumu
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amevipongeza vyama vinne vikuu vya siasa nchini ambavyo vimeanzisha majadiliano
ya kutafuta namna wajumbe waliosusia Bunge Maalum la Katiba wanavyoweza kurejea
Bungeni.
Aidha,
Rais Kikwete amewataka Watanzania kujiepusha na kishawishi cha kuingilia
mchakato wa Katiba Mpya kwa maneno na kutoa kauli nyingi, nyingine zikiwa za
upotoshaji na uchochezi, jambo ambalo linawanyima utulivu wajumbe wa Bunge
Maalum la Katiba.
Rais
Kikwete pia amewataka viongozi wa dini kuwaombea wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba
waliosusia mchakato wa kutafuta Katiba kurudi Bungeni ili kumaliza kazi ya
Kutunga Katiba Mpya kama wanavyotarajiwa na Watanzania.
Ili
kuhakikisha kuwa kazi hiyo ya Kutunga Katiba Mpya inakamilika bila wajumbe
kulazimika kufanya kazi hiyo kwa haraka kupita kiasi, Rais Kikwete ameliongezea
Bunge hilo maalum siku 60 za ziada kwa mujibu wa mamlaka ambayo anapewa na
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Rais
Kikwete ameyasema hayo leo, Jumapili, Julai 13, 2014 wakati alipohutubia mamia
kwa mamia ya waumini wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) kwenye
Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, katika maadhimisho la Kanisa hilo kutimiza miaka
75 tokea kuanzishwa nchini.
Katika
hotuba yake ambako amezungumzia masuala mbali mbali likiwemo lile la Katiba
Mpya, Rais Kikwete amewaambia wananchi waliofurika uwanjani humo:
“Bahati
nzuri wiki iliyopita, wawakilishi wa vyama vya CCM, CHADEMA,CUF na NCCR-Mageuzi
wamekuwa wanakutana kwa jitihada za Msajili wa Vyama vya Siasa. Naambiwa bado
wanaendelea na mazungumzo. Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati
kwa viongozi wa vyama hivyo kwa uamuzi wao
wa kukutana nakutafuta namna ya kusonga mbele. Tunatoa pongezi maalum
kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Mheshimiwa Jaji Mutungi kwa kufanya uamuzi
mzuri wa kuwakutanisha viongozi hao.”
Ameongeza
Rais Kikwete: “Wao ndio walitufikisha hapa na wao ndiyo wenye uwezo wa kutukwamua.
Wao wana ufuasi mkubwa miongoni mwa Wajumbe la Bunge Maalum.”
Amesema
Rais Kikwete: “Niwaombe Watanzania wenzangu
tuwape nafasi viongozi wetu wazungumze kwa utulivu. Tuache kwanza maneno maneno
yatakayowachanganya. Maana siku hizi wasemaji wamekuwa wengi na kauli zimekuwa
nyingi, nyingine zikiwa za upotoshaji na uchochezi . Miluzi mingi humchanganya
mbwa.”
Kuhusu
nafasi ya viongozi wa dini katika suala zima la baadhi ya watu kususia Bunge
Maalum la Katiba, Rais Kikwete amesema: “Ombi langu kwa nyie viongozi wa dini ni
kwamba tuwaombee ili warudi kukamilisha kazi tuliyowatuma. Tuwaombee wote
wafanye uamuzi wa pamoja. Sote tunataka warudi kukamilisha shughuli kwa sababu
mara ya mwisho lililobakia lilikuwa ni kupiga kura tu kuhusu kipengele cha
kwanza na cha sita cha Rasimu ya Katiba Mpya.”
Ameongeza:
“Tuwaombee
wawe na mazungumzo mazuri na yenye mafanikio. Wakubaliane juu ya kuendelea na
kukamilisha mchakato katika siku 60 za nyongeza kuanzia Agosti 5, mwaka huu,
2014. Tuombe kwa nguvu zetu zote ili Bwana Mungu awaongezee viongozi hao wapate
mwafaka utakaoliwezesha Taifa kupata Katiba nzuri na inayotekelezeka, katiba
yenye kuleta umoja, mshikamano na upendo, Katiba itakayodumisha amani na utulivu
nchini na kuchohcea maendeleo ya kasi zaidi.”
Akizungumzia
masikitiko ya Kanisa la TAG kuhusu kukwama kwa mchakato wa Katiba na rai ya
Kanisa hilo kuwataka wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kurejea Bungeni,
Rais Kikwete amesema:
“Masikitiko
yenu ndiyo masikitiko yangu na ndiyo masikitiko ya Watanzania wote. Rai yenu
ndiyo rai yangu na ya Watanzania wote. Nafarijika kusikia kuwa nanyi viongozi
wa dini mkizisihi pande zote kurejea Bungeni na kumaliza tofauti zao kwa mazungumzo
ndani ya Bunge.”
Sunday, July 13, 2014
KAMPUNI YA FARM EQUIPMENT (T) LIMITED ILIVYOPAMBA KONGAMANO LA KILIMO MVOMERO
Baadhi ya wakulima waliotembelea banda la Kampuni ya Farm Equip (T) Limited, wakati wa maonesho katika kongamano la mpango wa 'Matokeo Makubwa Sasa BRN' katika kilimo lililofanyika Kijiji chja Mkindo Tuliani mkoani Morogoro juzi, wakiangalia na kusikiliza maelezo kuhusu matumizi ya pambu za kupulizia dawa katika mashamba. Kushoto ni Meneja Mkuu wa kampuni hiyo. Naushad Khan.
Waziri wa Kilimo na Chakula, Mhandisi Christopher Chizza, (kulia juu ya mashine), akifurahi wakati akijaribu kuiendesha mashine ya kisasa ya kuvuna mpunga aina ya Kubota alipotembelea banda la Kampuni ya Farm Equip (T) Limited, wakati wa maonesho katika kongamano la mpango wa 'Matokeo Makubwa Sasa BRN' katika kilimo lililofanyika Kijiji chja Mkindo Tuliani mkoani Morogoro juzi. Chini (Kushoto) ni Meneja Mkuu wa kampuni hiyo. Naushad Khan.
Baadhi ya wakulima na wakazi wa Mvomero wakiangalia zana za kilimo aina ya Kubota na Sonalika zkatika banda ya la Kampuni ya Farm Equip (T) Limited wakati wa kongamano hilo
Waziri wa Kilimo akiendesha mashine ya kuvuna mazo aina ya Kubota ya Kwenye Banda la Farm Equip (T) Limited
RAIS JAKAYA KIKWETE AIAGIZA HALMASHAURI ZOTE NCHINI KUITENGEA NHC ARDHI
Na Mwandishi Maalumu
Rais
Kikwete amerejea Dar-es- Salaam mara baada ya majumuisho.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameziagiza Halmashauri zote nchini kutenga ardhi kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa ajili ya kujenga nyumba za bei nafuu kote Nchini.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameziagiza Halmashauri zote nchini kutenga ardhi kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa ajili ya kujenga nyumba za bei nafuu kote Nchini.
Rais
Kikwete ametoa maagizo hayo leo mjini Tanga wakati akifanya majumuisho ya ziara
yake katika Mkoa wa Tanga.
Rais amesema nyumba za bei nafuu zikijengwa zitatoa nafuu na kuondoa tatizo la makazi kwa wafanyakazi na wananchi wenye nia ya kumiliki nyumba na pia itapendezesha Halmashauri hizo.
Rais amesema nyumba za bei nafuu zikijengwa zitatoa nafuu na kuondoa tatizo la makazi kwa wafanyakazi na wananchi wenye nia ya kumiliki nyumba na pia itapendezesha Halmashauri hizo.
Katika
ziara yake ya kikazi Mkoani Tanga ambayo imefanyika kwa awamu mbili, Rais
ametembelea Wilaya zote za Handeni, Kilindi, Lushoto, Korogwe, Mkinga,
Muheza, Pangani na Tanga.
Rais
pia amewataka viongozi kote nchini kusimamia na kuhakikisha kuwa tatizo la
watoto kutomaliza shule linasimamiwa na kushughulikiwa ipasavyo kwa sababu huo
ndiyo msingi wa maendeleo katika Taifa letu.
"Viongozi
lazima kusimamia suala la elimu kwani hapo ndipo tunapowekeza kwa ajili ya
hatma ya vizazi vyote" amesema na kuongeza kuwa wasiokuwepo shule
watafutwe na wazazi waulizwe walipo watoto hao walioacha shule.
Rais
amezitaka Halmashauri zote zikae na kujadili hali ya mahudhurio ya watoto
shuleni na kutoa taarifa Serikali Kuu mapema.
Akiwa
Mkoani Tanga, Rais amesema Serikali itaendelea kutekeleza ahadi zake na
kusimamia zilizoanza ili zikamilike kwa wakati. Kuhusu uchaguzi wa Serikali za
Mitaa unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu, Rais Kikwete amesema hatma yake
iko katika matokeo ya maamuzi ya Bunge la Katiba na pia kutegemea aina gani ya
serikali itakayopendekezwa, ambapo kama Bunge la Katiba litaamua kuwa na Serikali
mbili, uchaguzi unaweza kusogezwa mbele kidogo kwa ajili ya matayarisho na
kisha kufanyika, ila kama itaamuliwa kuwa na Serikali tatu, uchaguzi huo
utategemea Katiba ya Tanganyika ambayo itabidi
iandikwe kwanza.
Thursday, July 10, 2014
VODACOM YAZINDUA HUDUMA MPYA NA MFUKO WA DHAMANA YA UWEKEZAJI TANZANIA (UTT)
Saimon Migangala wa UTT akizungumza wakati wa uzinduzi huo |
Salum Mwalim |
Wednesday, July 9, 2014
RAIS JAKAYA KIKWETE AAGIZA MA RC NA MA DC KUJENGA MAABARA KILA SEKONDARI IFIKAPO NOVEMBA MWAKA HUU
Na Mwandishi Maalumu
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kote nchini kuhakikisha
kuwa wanashirikiana na Wananchi kuhakikisha kuwa ifikapo Mwezi Novemba Mwaka
huu, kila Shule ya Sekondari katika maeneo yao, ina maabara kwa
ajili ya masomo ya Sayansi.
Rais
Kikwete amesema hayo Mkoani Tanga katika nyakati tofauti Wilayani Kilindi na
Lushoto ambapo yuko katika ziara ya kikazi Mkoani Tanga tangu tarehe 8 Julai
hadi tarehe 12 Julai,2014.
"Nataka
ifikapo Mwezi Novemba, Mwaka huu vyumba vya maabara viwe vimekamilika,
tulipeana miaka miwili, imetimia" Rais amesema
na kuongeza kuwa lazima tusahihishe makosa tuliyofanya ya kutojenga maabara
wakati tunajenga shule za sekondari nchini kote.
Mwaka
2006, Serikali ilihamasisha ujenzi wa Shule za Sekondari nchini kote na
muitikio ni mzuri, lakini hakukuwa na uhamasishaji wa kujenga maabara.
“Tumeamua
kushughulikia suala la maabara ili kuongeza idadi ya wanafunzi wa masomo ya Sayansi
kote nchini." Rais amesisitiza.
Rais
amesema ameridhika na upanuzi wa Elimu katika ngazi za Msingi na Sekondari kote
nchini na Serikali inaendelea na hatua ya kutatua changamoto za ubora wa Elimu,
kuongeza Walimu, kuongeza Vitabu, ujenzi wa Maabara na Nyumba za Walimu kote
nchini.
Akihutubia
katika mkutano wa hadhara Wilayani Lushoto Rais ameahidi kuboresha na
kushughulikia suala la ujenzi wa barabara ya kwenda Bumbuli na zaidi
kuhakikisha anaweka barabara ya lami katika mji wa Lushoto na mji mdogo wa
Bumbuli.
Rais
anaendelea na ziara Wilayani Lushoto na Mkinga ambapo anaendelea kuzindua miradi
na kukagua miradi ya maendeleo.
Subscribe to:
Posts (Atom)