Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi,
Mheshimiwa Waziri wa Fedha,
Waheshimiwa Manaibu Waziri,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam,
Mheshimiwa Balozi wa Uholanzi,
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,
Mheshimiwa M/kiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu
Waheshimiwa Wabunge na Madiwani,
Waheshimiwa Makatibu Wakuu,
Viongozi wa Vyama vya Siasa na Serikali,
Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi Mamlaka ya Viwanja vya Ndege,
Mkurugenzi Mkuu na Wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege,
Watendaji Wakuu kutoka Taasisi mbali mbali zilizoalikwa
Wadau wa Sekta ya Usafiri wa Anga,
Muwakilishi wa Benki ya HSBC,
Mtendaji Mkuu Benki ya CRDB,
Waandishi wa habari,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Ndugu wananchi na wageni waalikwa,
Kwanza
kabisa nimshukuru Waziri wa Uchukuzi na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam kwa kunialika katika hafla hii ya
kihistoria ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huu muhimu wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha
Julius Nyerere.
Nichukue fursa
hii pia kuupongeza Uongozi wa Wizara ya Uchukuzi, Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wote wa
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania kwa kazi nzuri ambazo wamekuwa wakizifanya
za kundeleza miundombinu ya viwanja vya ndege hapa nchini.
Ndugu wananchi na wageni waalikwa,
Kuanza kwa
ujenzi wa mradi huu ni muendelezo wa mafanikio makubwa ya utekelezaji wa ahadi
za Serikali ya Awamu ya Nne kama zilivyoianishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya
Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010. Serikali imedhamiria kwa dhati kabisa
kuendeleza na kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege.
Tunafanya
hivyo tukijua kuwa Usafiri wa Anga ni
usafiri wa leo, kesho na keshokutwa, nchi haiwezi kupata maendeleo kama hakuna
usafiri wa Anga. Lengo letu ni
kuhakikisha kuwa kiwanja hiki kinakua na kutoa fursa kwa
watanzania kwenda popote wakitokea hapa kwa shughuli
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwaongezea
uwezo zaidi wa kufanya biashara.
Ndugu wananchi na wageni waalikwa,
Katika
sekta ya huduma (service industries), viwanja vya ndege ni kati ya wawezeshaji
na watoa fursa namba moja. Kama tunavyofahamu Kiwanja hiki ndio lango kuu la
watu kuingia na kutoka nchini. Kwa mfano, mwaka jana 2013, Kiwanja hiki
kilihudumia wasafiri i zaidi ya milioni mbili na nusu. Hivyo ni matarajio yangu
kwamba kuboreshwa kwa kiwanja hiki kutaongeza uwezo wake wa kuhudumia abiria
wengi zaidi na kuwezesha ukuaji wa sekta nyingine hususan sekta ya utalii ambayo
inachangia kiasi kikubwa katika uchumi
wa taifa.
Kukamilika
kwa mradi huu wa jengo la tatu la abiria katika Kiwanja hiki cha Julius Nyerere
kitakuwa kichocheo cha uchumi kwa taifa na nchi jirani na hivyo kuvutia
wawekezaji wengi wa nchi za nje pamoja na wafanyabiashara kuleta ndege zao
kubwa zaidi. Jengo litakuwa kivutio kwa abiria kutokana na miundombinu yake
kuwa ya kisasa zaidi. Na zaidi ya hapo mradi utaongeza ajira kwa watanzania.
Nimeambiwa kuwa wakati wa ujenzi mradi utakuwa na wafanyakazi zaidi ya elfu
moja na utakapokamilika kiwanja cha ndege kitaongeza ajira kutoka 4000 wa sasa
hadi 6000. Rai yangu kwenu wananchi ni kuwa mchangamkie fursa za kibiashara na
kiuchumi zinazotokana na uwepo wa jengo hili jipya.
Ndugu wananchi na wageni waalikwa,
Mradi huu
ni muhimu sana kwa uchumi na taswira ya
nchi yetu na ambao watanzania wameusubiri kwa miaka mingi, hivyo Wizara ya Fedha
ihakikishe fedha za ujenzi zinapatikana na mradi uendelee na kukamilike kama
ilivyopanga. Wizara ya Uchukuzi kupitia Viwanja vya Ndege ihakikishe mradi huu
unasimamiwa vizuri kwa muda, kwa na kwa gharama zenye tija.
Napenda
kuwakikishia kwamba, jitihada hizi za Serikali hazitaishia katika kiwanja hiki
cha Julius Nyerere tu bali ni lengo letu kuona kwamba kila Mkoa unakuwa na
kiwanja cha ndege angalau kwa kiwango cha lami na kufungwa taa na vifaa vyote
muhimu ili kuweza kutoa huduma saa 24 katika kipindi chote cha majira ya mwaka.
Vilevile tutaendelea kujenga majengo ya abiria mazuri na ya kisasa yatakayowafanya
abiria kukaa na kupata huduma bila matatizo katika viwanja vyetu.
Ndugu wananchi na wageni waalikwa,
Sote
tumeshuhudia mafanikio makubwa ya kukua kwa sekta ya usafiri wa anga hapa
nchini, hivyo ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya viwanja vya ndege unapaswa
kwenda sambamba na ukuaji huo. Katika kipindi cha awamu ya nne Serikali imefanikiwa
kutekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi kwa kukamilisha kwa kiwango
kikubwa miradi ifuatayo:-
(a)
(b)
Ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege
cha Songwe chenye uwezo wa kuhudumia ndege ya ukubwa wa abiria ya 150 kwa
majira yote ya mwaka ambacho kimeanza kutumika na kurahisisha usafiri kwa mikoa
ya Mbeya, Njombe,Iringa, Rukwa na nchi jirani.
(c)
Ukarabati na upanuzi wa kiwanja
cha ndege cha Mpanda kwa kiwango cha lami ambacho kinaweza kuhudumia ndege ya
ukubwa wa kubeba abiria 70 kwa majira yote ya mwaka.
(d)
Ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha
ndege cha Kigoma kwa kiwango cha lami ambacho kitakapokamilika kitaweza
kuhudumia ndege za ukubwa wa kubeba abiria 150 kwa majira yote ya mwaka.
(e)
Ukarabati na upanuzi wa barabara
za kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha katika kiwanja cha ndege cha Tabora
ambacho sasa kinaweza kuhudumia ndege za ukubwa wa kubeba abiria 70 kwa majira
yote ya mwaka.
(f)
Ukarabati na upanuzi wa kiwanja
cha ndege cha Bukoba kwa kiwango cha lami ambacho kwa sasa kinauwezo wa
kuhudumia ndege za ukubwa wa kubeba abiria 50 kwa majira yote ya mwaka.
(g)
Kukamilika kwa ukarabati na
upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Mafia kwa kiwango cha lami ambacho kinaweza
kuhudumia ndege za ukubwa wa kubeba abiria 50 kwa majira yote ya mwaka.
Kutokana na jiografia ya Mafia kukamilika kwa kiwanja hicho ni ukombozi kwa
wananchi. Katika hali ya mvua nyingi zinazonyesha mwaka, kama hatungefanya
uboreshaji huo, Mafia ingetengwa kabisa na dunia kwani ndege zisingetua.
Utekelezaji wa miradi hii yote ni kuhakikisha kuwa
wananchi wanasafiri kwa urahisi na haraka
zaidi na pia kuwawezesha kufanya
biashara kwa ufanisi zaidi ili kuinua
vipato vyao.
Ndugu wananchi,
Dhamira
hii nzuri ya Serikali ya kuboresha miundombinu ya viwanja vyetu vya ndege haitaweza
kufanikiwa bila kupata ushirikiano kutoka kwa wananchi hasa wale waishio jirani
na maeneo ya viwanja hivi. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru na
kuwapongeza wananchi wote ambao walikuwa
wakazi wa eneo hili la Kipawa na
Kigilagila ambako leo mradi huu unafanyika, kwa kutoa ushirikiano wa hali ya
juu kwa Serikali kwa kukubali kuhama kutoka katika eneo hili kupisha upanuzi wa
mradi huu. Natoa rai kwa wananchi wa
maeneo mengine ambayo yatahitajika kwa miradi kama hii ya
kimaendelea kuiga mfano wa wenzao wa Kipawa na Kigilagila.
Lakini
hata baada ya miundombinu hii ya viwanja kukamilika bado tunahitaji ushirikiano
wa wananchi katika kuhakikisha kuwa miundombinu hiyo inalindwa na mipaka yake
haivamiwi. Nichukue nafasi hii kutoa tahadhari kwa wale ambao wamekuwa na tabia
ya kuvamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya ndege kwa
lengo la kutegemea kulipwa fidia waache tabia
hiyo, vinginevyo Mamlaka husika zisisite kuwachukulia hatua za kisheria na
kuwaondoa mara moja watu kama hao.
Natambua
kwamba tatizo hili la uvamizi wa maeneo ya viwanja kwa kiasi kikubwa
linachangiwa na utaratibu uliokuwepo kwa miaka mingi wa kuyaacha maeneo
haya bila hati miliki. Nafurahi kusikia
kwamba Wizara ya Uchukuzi kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imeliona tatizo
hilo na kuamua kulitafutia ufumbuzi kwa kufuatilia hati miliki ya maeneo hayo
yalitotengwa kwa viwanja vya ndege ambapo kwa sasa viwanja vya Julius Nyerere,
Arusha, Kilimanjaro, Bukoba, Musoma, Moshi, Tanga na Kigoma tayari mchakato wa
hati miliki umekamilik. Tafadhali mchakato huu uendelee kwa viwanja vyote na
naziagiaza Mamalaka husika za Ardhi kutoa ushirikiano katika kufanikisha suala
hilo.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana.
Kuhusu
changamoto zinazowakabili katika uendeshaji wa viwanja vya ndege, napenda
kuwapongezeni Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harison Mwakyembe, Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege pamoja na taasisi zote zenye jukumu la ulinzi na usalama kwa
kusimamia suala la udhibiti wa upitishaji wa madawa ya kulevya ambapo kwa kiasi
kikubwa limedhibitiwa.
Pamoja na
mafanikio haya ni muhimu viwanja vya ndege vikatoa huduma bora zaidi ili viweze
kushindana na viwanja vingine duniani kwa kuweka taratibu za uendeshaji na
menejimenti zinazolingana na viwanja vingine vya kimataifa. Hivyo naagiza Wizara
zote zenye taasisi katika viwanja vya ndege kushirikiana kuweka kanuni na taratibu
zitakazoondoa changamoto nyingi na misuguano ya uendeshaji wa viwanja vya ndege
.
Baada ya
kusema haya, sasa niko tayari kuweka jiwe la msingi la mradi huu wa ujenzi wa
jengo la tatu la abiria. Napnda kuwatakia kazi njema ya kukamisha mradi huu kwa
wakati, kwa viwango na kwa gharama yenye thamani ya pesa.
ASANTENI
SANA.
No comments:
Post a Comment