Na Mwandishi Maalumu
RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametumia
siku nzima ya Ijumaa, Mei 9, 2014, kutembelea kiwanda kikubwa zaidi cha saruji
kuliko kingine chochote duniani cha Dangote Cement Obajana Plant na
kinachomilikiwa na tajiri mkubwa zaidi wa Afrika, Bw. Aliko Dangote, ambaye
pia anajenga kiwanda kikubwa cha saruji Mjini Mtwara.
Akiandamana
na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Abdallah Kigoda, kwa siku nzima,
Rais Kikwete ametembelea kiwanda hicho cha Saruji cha Dangote kilichoko katika
eneo la Obajana, Jimbo la Kogi, kilomita
400 kaskazini mashariki mwa mji maarufu wa kibiashara wa Nigeria, Lagos.
Rais
Kikwete ambaye alikuwa nchini Nigeria kuhudhuria Kongamano la Uchumi
Duniani-Afrika (WEFA) mwaka huu aliamua kutumia siku yake ya mwisho ya ziara
yake ya siku tatu nchini humo, kwa kutembelea uwekezaji mkubwa wa mwekezaji
ambaye ameanza ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Mtwara ambacho kitakuwa kiwanda
kikubwa zaidi cha saruji kuliko kingine chochote katika Tanzania, kikiwa na
uwezo wa kuzalisha tani za kimetriki milioni tatu kwa mwaka.
Rais
Kikwete ambaye amepokelewa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kiwanda hicho na Bwana
Dangote mwenyewe, ameanza ziara yake kwa kutembelea machimbo ya kiwanda hicho
ambayo yako kilomita tisa kutoka kiwandani ambako malighafi ya kiwanda hicho
husafirishwa kwa madaraja na mikada maalum hadi kiwandani.
Bw.
Dangote amemwambia Rais Kikwete kuwa kwa sasa Kiwanda cha Obajana kinazalisha
tani za kimetriki milioni 10.25 kwa sasa kwa mwaka na hivyo kukifanya kiwanda hicho
kuwa kiwanda kikubwa zaidi cha saruji duniani kilichoko katika eneo moja na
kuwa baada ya upanuzi unaoendelea kufanywa kwenye kiwanda hicho, uwezo wake wa
uzalishaji utaongezeka na kufikia tani za kimetriki 13.0 kwa mwaka ifikapo
mwakani 2015.
Dangote amemwambia Rais Kikwete kuwa kiwanda hicho kilicho kwenye eneo la
kilomita za mraba saba kitakuwa kimegharimu kiasi cha dola za Marekani bilioni
2.5 wakati upanuzi wake utakapokamilika. Kwa sasa kiwanda hicho kina biashara
ya dola za Marekani bilioni mbili kwa mwaka.
Mfanyabiashara huyo amemwambia Rais Kikwete kuwa kiwanda hicho kilichoanza kujengwa mwaka
2003 na kukamilishwa mwaka 2006 na hatimaye kuzinduliwa na Rais Olusegun
Obasanjo Mei 12, mwaka 2007, wiki mbili kabla ya kustaafu Urais wa Nigeria,
kinaajiri watu 800 kwa wakati mmoja na hivyo kuwa miongoni mwa waajiri wakubwa
zaidi katika Nigeria.
“Mheshimiwa
Rais, ili kuelewa vizuri mchango wa kiuchumi na kijamii wa kiwanda hiki na
viwanda vyetu vingine katika maeneo mengine ya Nigeria, unahitaji kukumbuka
kuwa kabla ya kuanza kujenga kiwanda hiki, Nigeria nzima ilikuwa na uwezo za
kuwazalisha tani za kimetriki za saruji milioni1.5 tu, wakati huo chini ya
miaka 10 iliyopita. Tunataka kufikia hatua ya kuhakikisha kuwa eneo la Afrika
Magharibi na hata Bara letu la Afrika linaacha kabisa kuagiza saruji nje ya
Bara letu. Na tutafikia huko.”
Mbali
na Kiwanda cha Obajana, Kampuni ya Saruji ya Dangote inazalisha saruji katika
maeneo mengine mawili ya Nigeria ambapo uzalishaji wa jumla wa maeneo hayo
matatu ni tani za metriki 20.25 kwa mwaka.
Amesema
Bwana Dangote kuwa ili kuweza kuwa na uhakika wa umeme, uongozi wa kiwanda
hicho uliamua kuzalisha umeme wake kwa ajili ya kiwanda hicho kwa kujenga, miongoni
mwa hatua nyingine, bomba la kilomita 92 la kusafirisha gesi kutoka Ajaokuta
hadi kwenye kiwanda hicho.
Alipoulizwa
na Rais Kikwete kama wanategemea kwa namna yoyote umeme wa taifa, Bwana Dangote
alijibu kwa furaha, “hatujaunganishwa kwenye gridi ya taifa na tunadhani hili ni jambo zuri
kwa sababu hatua tulizochukua zinatuhakikishia umeme wakati wote na kwa kiwango
ambacho tunakihitaji. Tunatumia gesi ama diseli yetu wenyewe. Na wala siyo
umeme tu, hata miundombinu ya eneo hilo likiwemo daraja hili kubwa
linalonganisha eneo la machimbi na kiwanda, tumejenga sisi Mheshimiwa Rais.”
amesema kuwa mbali na kujenga miundombinu ya umeme wake, kiwanda hicho
pia kimejenga bwawa lake lenyewe kwa ajili ya huduma ya maji kusaidia
uzalishaji wa saruji bila kutegemea huduma ya maji ya Serikali. Aidha, bwawa
hilo linatoa huduma ya maji kwa jamii inayozunguka kiwanda hicho.
Mbali
na shughuli za kiwanda, Kampuni ya Bwana Dangote inashiriki kwa karibu sana
shughuli za jamii inayozunguka kiwanda ambacho kwa sasa imeanzishwa miji midogo
saba katika eneo lililokuwa pori lenye nyumba 50 za wenyeji tu kabla ya
shughuli za kiwanda hicho kuanzishwa.
Pia amemwambia Rais Kikwete kuwa kampuni yake inatoa shughuli za elimu,
maji na umeme kwa wananchi ambao wanazunguka kiwanda ambacho tokea kuanzishwa
kwake limevutia mabenki 13 ambayo yameanzishwa matawi yake katika eneo la
kiwanda. “Mheshimiwa Rais, mbali na nyumba za wafanyakazi, tunawajengea hata
nyumba za kuishi wananchi wanaozunguka eneo hili ambao wanatuunga mkono sana.”
Mbali
na kutoa huduma nyingine za kijamii, Kampuni ya Saruji ya Dangote inajenga
taasisi kubwa ya elimu ya Dangote Academy ambayo itatoa elimu na mafunzo ya
kiufundi kwa ajili ya kuandaa wafanyakazi wa kiwanda hicho na watoto wa jamii
inayozunguka kiwanda hicho.
Ili
kuhakikisha kuwa upanuzi wa kiwanda hicho unakwenda kwa kasi kubwa zaidi, Bw.
Dangote ameagiza kiasi cha malori 6,000 kutoka China kusaidia ujenzi na pia
amechukua uamuzi usiokuwa wa kawaida wa kuagiza maelfu ya vibarua kutoka nchi
hiyo hiyo ya China kushiriki katika ujenzi huo na kuumaliza kwa haraka.
Alisema kampuni yake inafanya jitihada kubwa
kuhakikisha kuwa Rais Kikwete
anakifungua kiwanda cha saruji cha Mtwara kabla ya kustaafu mwishoni mwa mwaka
ujao.
Mbali
na Nigeria na Tanzania, Bw Dangote ana viwanda ama anajenga viwanda vya
saruji ama na shughuli za saruji katika nchi 14 za Afrika ikiwamo Ethiopia,
Zambia, Mozambique, Kenya, Senegal na Sierra Leone, Afrika Kusini, Congo
(Brazzaville), Cameroun, Ghana, Liberia na Ivory Coast.
Mbali
na shughuli za uzalishaji wa saruji, Dangote ambaye anakubaliwa kuwa
tajiri mkubwa zaidi katika Afrika kwa thamani ya dola za Marekani bilioni 25
yeye na kampuni yake ya Dangote Group pia ina shughuli za uzalishaji wa sukari,
uzalishaji wa chumvi, utengenezaji wa magunia, uzalishaji maji, uzalishaji wa
vyakula vya aina mbalimbali, uzalishaji wa mafuta ya kupikia, utengenezaji wa
nyanya. Kwa sasa anaendelea na ujenzi wa kiwanda cha mbolea na kile cha
kuzalisha bidhaa za petrol na kemikali.
Kampuni
ya Saruji ya Dangote – Dangote Cement- ndiyo kampuni kubwa kuliko zote katika
Afrika Magharibi kwa sasa ikiwa na thamani ya dola za Marekani bilioni 22.7 kwa
tathmini ya mwaka huu baada ya kuongeza thamani yake kutoka dola za Marekani
bilioni14.5 za mwaka jana.
Mwishoni
mwa ziara hiyo yenye mafanikio makubwa, Rais Kikwete ameondoka Obajana kurejea
nyumbani kupitia Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Luanda, Angola
ambako kesho (jumamosi) anatarajia kukutana na marais wa nchi hiyo kabla ya
kurejea nyumbani.
No comments:
Post a Comment