Sunday, May 25, 2014

RAIS JAKAYA KIKWETE AMLILIA MAXIMILLIAN WA MLIMANI TV


TAARIFA MAALUMU 
 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari Mheshimiwa Dkt.Fenella Mukangara kufuatia kifo cha Mpigapicha wa kituo cha television cha Mlimani, Ndugu Maximilian John kilichotokea alfajiri ya kuamkia tarehe 24 Mei,2014..

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Maximilian kilichotokana na maradhi ya moyo, Sukari  na shinikizo la damu. Kifo hicho ni pigo na pengo kubwa kwa tasnia ya habari hapa nchini,”Amesema  Rais Kikwete katika salamu hizo.
“Bw. Maximilian atakumbukwa kwa uchapakazi wake na uhodari katika kazi zake siku zote. Kifo ni maandiko ya Mwenyezi Mungu hivyo hatuna budi kumshukuru kwa yote.


“Nakutumia salamu zangu za dhati kuomboleza msiba huu. Aidha, kupitiakwako, naitumia familia ya Ndugu Maximilian, pole za dhati ya moyo wangu kwa kuondokewa na mzazi na mhimili wa familia. Aidha, salamu hizi ziwafikie pia wanahabari wote, wafanyakazi wenzake, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu. Nakuomba uwajulishe kuwa naelewa machungu yao katika kipindi hiki na nawaombea subira na uvumilivu. Ninaungana nao kumwomba Mwenyezi  Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke peponi roho ya marehemu. Amen,” amesema Rais katika salamu hizo.


Ndugu Maximilian John ameacha mke na watoto wanne.

No comments:

Post a Comment