Na Mwandishi Maalumu
MJUMBE
Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu ya Kimataifa – UN Special Envoy for Global
Education - na Waziri Mkuu wa
zamani wa Uingereza, Mheshimiwa Gordon Brown amesema kuwa Tanzania imefanya
vizuri zaidi kuliko nchi nyingine yoyote ya Afrika katika uandikishaji wa watoto kuanza
shule.
Aidha,
Mheshimiwa Brown amesema kuwa hana uhakika kama Watanzania wanajua fika kuwa
nchi yao imefikia mafanikio makubwa mno ya elimu ambayo bado ni ndoto tu kwa
nyingine nyingi za Afrika.
Kwa
sababu hiyo na kwa sababu ya mafaniko hayo, Mheshimiwa Brown amesema kuwa Umoja
wa Mataifa na taasisi zake na nyingine za kimataifa ziko tayari kuisaidia
Tanzania kufikia lengo la kusajili watoto wote kwa asilimia 100 ya watoto wote
wanaotakiwa kuingia shule katika muda wa uongozi wa Rais Kikwete na kabla
hajaondoka madarakani mwishoni mwa mwaka ujao.
“Mheshimiwa
Rais, tunapenda kukupongeza kwa kufanya vizuri sana katika nyanja ya elimu. Haya
ni mafanikio ya uongozi wako. Umewezesha asilimia 98 ya watoto wanaotakiwa
kuanza shule kuingia shule. Hakuna nchi nyingine ya Afrika ambayo imefikia
mafanikio kiasi hiki. Tunapenda kukusaidia na kufanya kazi na wewe ili tufikie
asilimia 100, “
amesema
Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Uingereza katika mkutano na Rais Kikwete.
Rais
Kikwete na Mheshimiwa Brown wamekutana kwenye Hoteli ya Hilton mjini Abuja
ambako wote wawili wanakaa wakati wanahudhuria Kongamano la Uchumi Duniani –
kwa Bara la Afrika lilioanza leo, Jumatano, Mei 7, 2014 katika mji mkuu wa
Nigeria.
Ameongeza
Mheshimiwa Brown, “Mheshimiwa Rais, sasa tunataka kusaidia kuwapeleka shule kiasi cha
watoto 100,000 ambao ni asilimia mbili ambao kwa sasa hawaendi shule. Tunajua
hawa ni watoto wa makabila ya wafugaji ambao wanahamahama kila siku na mifugo
yao na watoto wao vile vile. Lakini Serikali yako imepiga hatua kubwa, kubwa
kuliko inavyofikiriwa na mataifa mengine ya Afrika katika kukabiliana na hali
hiyo.”
Mheshimiwa
Gordon Brown pia amesema kuwa Umoja wa Mataifa na taasisi zake ziko tayari
kuisaidia Tanzania katika kuboresha ufundishaji wa masomo ya sayansi ambayo
hayana walimu wa kutosha katika Tanzania na duniani pote kwa kutumia njia za
ufundishaji za kutumia teknolojia ya habari, mawasiliano na teknolojia.
Rais Kikwete pia amekutana na kufanya mazungumzo na Bwana Mark Suzman, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Taasisi ya Bill and Melinda Gates ya Marekani. Aidha, Rais amekutana na kufanya mazunguzo na Bwana Sunnil Bharti Mittal, Mwenyekiti wa Kampuni ya kimataifa ya simu ya Airtel duniani.
No comments:
Post a Comment